EU yayataja makubaliano ya nyuklia ya Iran kama 'hatua kubwa'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28894-eu_yayataja_makubaliano_ya_nyuklia_ya_iran_kama_'hatua_kubwa'
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ametoa wito wa kuungwa mkono na kutekelezwa ipasavyo makubaliano ya nyuklia ya Vienna sambamba na kukabiliana na hatua yoyote ya kukwamisha utekelezaji wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2017 03:08 UTC
  • EU yayataja makubaliano ya nyuklia ya Iran kama 'hatua kubwa'

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ametoa wito wa kuungwa mkono na kutekelezwa ipasavyo makubaliano ya nyuklia ya Vienna sambamba na kukabiliana na hatua yoyote ya kukwamisha utekelezaji wake.

Katika hotuba yake ya kila mwaka mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana, Federica Mogherini ameyataja makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kama hatua kubwa na muhimu na kusisitiza kuwa yanaweza kutumia kama kigezo katika kupatia ufumbuzi migogoro mbali mbali ya kimataifa kupitia njia za kidiplomasia.

Mogherini amesema: "Makubaliano ya nyuklia ya Iran yamezifungulia njia nchi za Ulaya. Kuna haja ya pande zote husika kuuheshimu na kutekeleza muafaka huo."

Maafisa wa ngazi za juu walioshiriki mazungumzo ya nyuklia huko Vienna

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa EU amesema makubaliano hayo yaliidhinishwa na kupata baraka za Baraza la Usalama la UN na hivyo ni muafaka wa jamii yote ya kimataifa na wala sio wa watu wachache walioshiriki mazungumzo ya kabla ya kufikia makubaliano hayo.

Itakumbukwa kuwa, baada ya mazungumzo yaliyochukua muda mrefu, Marekani na washirika wake wa Ulaya pamoja na Russia na China kupitia kundi la 5+1, Julai mwaka 2015 zilifikia muafaka wa nyuklia na Iran uliojulikana kama JCPOA, ambao unatoa hakikisho la kuendelezwa shughuli za amani za nyuklia za Iran. 

EU imekuwa ikimtadhadharisha Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya kukiuka makubaliano hayo na madhara makubwa yatakayosababishwa na hatua hiyo.