Umoja wa Mataifa wataka wakimbizi wa Somalia wasaidiwe
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetoa wito wa kusaidiwa wakimbizi wa Somalia ambao kwa sasa wanahitajia misaada ya haraka kutokana na hali mbaya wanayokabiliwa nayo.
Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, ili kudhamini mahitaji ya wakimbizi wa Somalia ndani ya nchi hiyo na katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki, inahitajia dola milioni 488.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetahadharisha kwamba, endapo misaada hiyo haitawafikia wakimbizi hao kwa wakati, kuna uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema, Wasomali milioni 6 wanahitajia misaada ya haraka sana ya kibinadamu wakiwemo watoto wadogo zaidi ya laki 2 na 75 elfu, wanaosumbuliwa na utapiamlo na lishe duni.
Aidha Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia akihutubia katika mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia uliofanyika mjini London Uingereza kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo alisema kuwa, nchi yake inahitajia msaada wa kimataifa katika jitihada zake za kuwaletea ustawi wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Zaidi ya Wasomali milioni mbili walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na mgogoro wa kibinaadamu ulioikumba nchi yao ambapo zaidi ya watu milioni moja wamekuwa wakimbizi ndani ya taifa hilo la Pembe ya Afrika.