Human Rights Watch yamuonya Trump kuhusu kuiuzia silaha Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29400-human_rights_watch_yamuonya_trump_kuhusu_kuiuzia_silaha_saudia
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limemuona Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na kuiuzia silaha Saudi Arabia kutokana na nchi hiyo kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2017 23:27 UTC
  • Human Rights Watch yamuonya Trump kuhusu kuiuzia silaha Saudia

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limemuona Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na kuiuzia silaha Saudi Arabia kutokana na nchi hiyo kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeonya katika ripoti yake yenye anwani inayosema "Kuongezeka Usafirishaji Silaha, Zawadi ya Trump kwa Jinai za Saudia Yemen" kwamba, kuendelea hatua ya Marekani ya kuiuzia silaha nchi ambayo imekiuka mara chungu nzima sheria za vita itafuatiwa na majukumu ya kisheria kwa viongozi wa Marekani kutokana na kuchochea na kusaidia jinai za kivita.

Sambamba na safari ya Rais Donald Trump nchini Saudia, taasisi hiyo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu imemtaka rais huyo wa Marekani awatake watawala wa Riyadh wabadilishe muamala wao katika hujuma na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen.

Watoto wa Yemen wanauawa kila siku na mashambulio ya Saudia

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Ikulu ya Marekani White House imetangaza habari ya kutiwa saini mkataba wa silaha wenye thamani ya dola bilioni 460 kati ya Riyadh na Washington katika safari ya Rais Trump nchini Saudi Arabia.

Huku hayo yakiripotiwa Saudia imeendelea kufanya mauaji dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen kutokana na kuendelea hujuma na mashambulio yake ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo ambayo yamesababisha pia uharibifu mkubwa.

Itakumbukwa kuwa Saudia ilianzisha hujuma dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutoroka nchi.