UN yaeleza wasi wasi wake kuhusu hali ya mateka wa Palestina
Umoja wa Mataifa umeeleza wasi wasi wake kuhusu hali ya kiafya ya mateka wa Kipalestina waliosusia chakula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Zeid Ra’ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo amesema kuwa binafsi ameshtushwa na hali mbaya wanayopitia wafungwa wa Kipalestina katika magareza ya Israel na hususan mateka hao kuzuiwa kuonana na mawakili wao au hata kutembelewa na familia zao.
Amesema kwa mujibu wa sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu, kila mfungwa ana haki ya kufanya mazungumzo na kushauriana na wakili wake na haki hiyo haifai kukiukwa kivyovyote vile.
Kadhalika afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza masikitiko yake kuhusu hali ya kiafya ya mamia ya wafungwa hao katika jela za kutisha za utawala haramu wa Israel.
Hii ni katika hali ambayo, mateka wasiopungua 60 wa Kipalestina miongoni mwa maelfu ya wafungwa hao waliosusia kula chakula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wamehamishiwa hospitalini baada ya hali zao kuzidi kuwa mbaya.
Awali idadi ya wafungwa waliosusia kula ilikuwa 700, lakini baada ya muda, malalamiko dhidi ya hali mbaya waliyonayo wafungwa hao na kutoshughulikiwa hali zao za kiafya pamoja na haki zao yalishamiri, ambapo kwa sasa idadi ya wafungwa Wapalestina waliosusia kula imefikia 2,000.