Gaidi aua Waislamu wawili kwa sababu ya Hijabu nchini Marekani
Waislamu wengine wawili wameuawa nchini Marekani ikiwa ni muendelezo wa ukandamizaji na unyanyasaji wa Waislamu hususan tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Gaidi moja aliyekuwa na silaha amewashambulia Waislamu kadhaa na kuua wawili na kujeruhi wengine watatu baada ya kutoa matusi makali dhidi ya wanawake wawili waliokuwa wamevaa Hijabu ndani ya treni ya mji wa Portland katika jimbo la Oregon nchini Marekani.
Gaidi huyo mwenye umri wa miaka 35 ana historia ya kufanya jinai, na baada ya kufanya mauaji hayo ya kigaidi ametoroka bila ya kukamatwa na polisi.
Watu walioshuhudia ugaidi huo wamesema kuwa, gaidi huyo ana historia ya kuwatukana Waislamu mara kwa mara na amekuwa akitoa maneno ya kibaguzi dhidi ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Kabla ya hapo pia, kulikuwa kumetangazwa habari ya mtu mmoja kumshambulia binti wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 14 kaskazini mwa mji wa Atlanta katika jimbo la Georgia nchni Marekani.
Binti huyo wa Kiislamu alishambuliwa na mtu huyo mwenye chuki za kidini wakati alipokuwa ananunua vitu katika duka moja kubwa. Mtu huyo alimvua Hijabu binti huyo wa Kiislamu na kumwita gaidi.
Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani limesema kuwa chuki zote hizo dhidi ya Waislamu zimeongezeka kutokana na uchochezi na matamshi ya kiuadui ya rais wa Marekani, Donald Trump.