Amnesty yashutumu uamuzi wa Saudia na wapambe wake dhidi ya Qatar
(last modified Tue, 13 Jun 2017 13:56:25 GMT )
Jun 13, 2017 13:56 UTC
  • Amnesty yashutumu uamuzi wa Saudia na wapambe wake dhidi ya Qatar

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa vikali hatua zisizo na mantiki za Saudi Arabia na wapambe wake dhidi ya Qatar.

Shutuma hizo zimetolewa na Salil Shetty, Katibu Mkuu wa Amnesty International katika mkutano wake na Ali Bin Smaikh al-Marri, Mwenyekiti wa Kamati Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar na kuongeza kuwa, vikwazo na vizingiti vilivyowekwa na Riyadh na wapambe wake dhidi ya raia wa Qatar vinakiuka moja kwa moja haki za binadamu zilizoanishwa kwenye hati na sheria za kimataifa.

Shetty amezitaka asasi zote husika za kimataifa kuchukua hatua za dharura kuzuia utekelezwaji wa vikwazo hivyo. Katibu Mkuu wa Amnesty International amesema ujumbe kutoka shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu umerekodi kesi 700 zinazoashiria ukiukaji wa haki za msingi za raia wa Qatar kutokana na mgogoro huo ulioanzishwa na Saudia na baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi dhidi ya Doha.

Meli ya shehena za chakula ya Iran kwa ajili ya Qatar. Saudia imefunga mpaka wa nchi kavu na Qatar

Qatar kupitia Waziri wa Mambo ya Nje imevitaja vikwazo vya Saudi Arabia na waitifaki wa Riyadh dhidi ya Doha kuwa si vya kiadilifu na vilivyo kinyume cha sheria.

Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri tarehe 5 mwezi huu zilitangaza kusitisha uhusiano wao wa kidiplomasia na kibiashara na Qatar zikidai kuwa Doha inayaunga mkono makundi yenye misimamo mikali, tuhuma ambazo Qatar imeyakanusha vikali. Kadhalika baadhi ya nchi za Kiafrika zimefuata kibubusa msimamo huo wa Saudia na kutangaza kukata au kupunguza uhusiano wao na Doha.  

 

Tags