Jeshi la Yemen lalipiza kisasi na kuua wanajeshi wanne Wasaudi
Wanajeshi wanne wa Saudi Arabia wameuawa katika oparesheni ya pamoja ya kulipiza kisasi ya Jeshi la Yemen na wapiganaji wa Ansarullah katika eneo la Asir ndani ya ardhi ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al Masirah, katika oparesheni hiyo ya Jumanne alasiri, Jeshi la Yemen na waitifaki wake wametekeleza oparesheni na kushambulia eneo la mpakani la al-Alab na kuwaua wanajeshi hao wa dola vamizi la Saudia. Aidha wanajeshi wa Yemen na wapiganaji wa Ansarullah wamevurumisha mizinga katika kituo cha kijeshi cha al-Makhrouq katika eneo la Najran yapata kilomita 844 kusini mwa mji mkuu Riyadh. Ripoti iliyochapishwa na Shirika la Reuters mwaka jana ilisema zaidi ya wanajeshi 400 walikuwa wameshauawa tokea vita vya Yemen vianze Machi mwaka 2015. Tokea ianze hujuma ya Saudia, askari wa Jeshi la Yemen wakishirikiana na wapiganaji wa Ansarullah wamekuwa wakiilinda nchi hiyo pamoja na kuwa hawana suhula za kutosha za kijeshi.
Saudia iliivamia Yemen kwa himya ya Marekani kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Raia zaidi ya elfu 13 wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukishindwa kuchukua hatua yoyote ya kuzuia jinai hizo za Saudia huko Yemen.