Antonio Guterres aipongeza Iran kwa kufungamana kikamilifu na JCPOA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kufungamana kwake kikamilifu na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Antonio Guterres amesema hayo kwa mnasaba wa kutimia miaka miwili tangu kutiwa saini makubaliano hayo ya nyuklia kati ya Iran na madola sita makubwa duniani yaani nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani au kundi la 5+1.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameisifu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kuheshimu kwake na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo aliyoyataja kuwa ni mafanikio makubwa.
Aidha Guterres amezitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ziendelee kuunga mkono
utekelezwaji wa makubaliano hayo ya nyuklia kwa mujibu wa azimio nambari 2231 na maamuzi mengine ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataiga yanayohusiana na makubaliano hayo.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 14 Julai mwaka 2015 Iran na madola sita makubwa yalitiliana saini makubaliano ya nyuklia kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya mazungumzo magumu na ya muda mrefu. Tarehe 20 Julai mwaka huo huo, makubaliano hayo yalipasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwa hati ya kimataifa. Pamoja na mafanikio hayo, Marekani imeendelea kulaumiwa kutokana na kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo.