Seneta aliyeikejeli burqa Bungeni huko Australia akosolewa vikali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33300-seneta_aliyeikejeli_burqa_bungeni_huko_australia_akosolewa_vikali
Seneta aliyeingia Bungeni akiwa amevalia burqa kwa kejeli na dhihaki nchini Australia amekosolewa vikali na Mwanasheria Mkuu na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kwa kuvunjia heshima vazi hilo linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Aug 18, 2017 08:15 UTC
  • Seneta aliyeikejeli burqa Bungeni huko Australia akosolewa vikali

Seneta aliyeingia Bungeni akiwa amevalia burqa kwa kejeli na dhihaki nchini Australia amekosolewa vikali na Mwanasheria Mkuu na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kwa kuvunjia heshima vazi hilo linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu.

Pauline Hanson, ambaye ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha One Nation jana Alkhamisi aliingia Bungeni akiwa amevalia burqa huku maseneta wa chama chake wakicheka kwa dharau.

Inaarifiwa kuwa alichukua hatua hiyo ili kumshinikiza Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo apasishe na kuwa sheria muswada wa kupiga marufuku vazi hilo nchini humo. Hata hivyo George Brandis, Mwanasheria Mkuu wa Australia alimkosoa vikali seneta huyo na kusema kuwa: "Seneta Hanson, sote tunafahamu wewe sio Mwislamu, kuwa makini sana usikejeli dini za watu wengine."

Matamshi ya Brandis yameungwa mkono na Malcolm Turnbull, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, aliyesema kuwa Mwansheria Mkuu amezungumza kwa ufasaha na busara kukosoa kitendo hicho cha chuki cha Seneta Hanson.

Seneta Hanson akivua burqa kwa kejeli

Septemba mwaka jana, Seneta Hanson alikosolewa vikali kwa matamshi yake yaliyojaa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, baada ya kusema kuwa, Australia ipo katika hatari ya kufurika Waislamu na eti uhalifu ni mwingi katika maeneo wanamoishi wafuasi wa dini hiyo nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa mwaka jana na Idara ya Takwimu nchini Australia yanaonyesha kwamba, idadi ya watu wenye hamu ya kuingia kwenye dini nyingine zisizo Ukristo ikiwemo dini tukufu ya Kiislamu imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mabinti wa Kiislamu nchini Australia

Matokeo hayo yameonesha kuwa, katika kipindi cha kati ya miaka 1991 na 2016 kasi ya watu kuelekea kwenye dini ya Uislamu imepanda kwa asilimia 160.