Ongezeko kubwa la kujiua wanachuo lawatia wasiwasi viongozi wa Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33877-ongezeko_kubwa_la_kujiua_wanachuo_lawatia_wasiwasi_viongozi_wa_uingereza
Taasisi moja ya nchini Uingereza imetangaza habari ya kuongezeka kupindukia kesi za kujiua na matatizo ya kiakili na kisaikolojia kati ya wanafunzi vya vyuo katika miaka ya hivi karibuni nchini humo.
(last modified 2025-11-09T00:45:59+00:00 )
Sep 02, 2017 14:49 UTC
  • Ongezeko kubwa la kujiua wanachuo lawatia wasiwasi viongozi wa Uingereza

Taasisi moja ya nchini Uingereza imetangaza habari ya kuongezeka kupindukia kesi za kujiua na matatizo ya kiakili na kisaikolojia kati ya wanafunzi vya vyuo katika miaka ya hivi karibuni nchini humo.

Gazeti la The Guardian linalochapishwa mjini London limenukuu ripoti ya kituo cha utafiti na uwekaji sera za umma cha Uingereza inayosema kuwa, wanachuo 134 wa vyuo vikuu mbalimbali vya Uingereza walijiua mwaka 2015 na hiyo ni idadi kubwa ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, idadi kubwa sana ya wanachuo wamekumbwa na matatizo ya kiakili kutokana na madeni makubwa ya fedha ya kugharamia masomo yao.

Uchunguzi wa taasisi hiyo muhimu unaonesha kuwa, idadi ya wanachuo wa mwaka wa kwanza waliotangaza matatizo yao ya kiakili imeongezeka mara tano ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.

Kukata tamaa ni moja ya sababu za watu kujiua barani Ulaya

Wanafunzi wa kike ndio wanaounda idadi kubwa ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliotangaza matatizo yao ya kiakili na kisaikolojia.

Mwito wa kuweko washauri wa kisaikolojia kwenye vyuo vikuu vya Uingereza umeongezeka kwa asilimia 94 ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.

Mark Salter, msemaji wa chuo cha kifalme cha masuala ya saikolojia nchini Uingereza kinachojulikana kwa jina la Global Health for Public Health England amesema kesi za kujiua wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo zimeongezeka mara mbili ikilinganishwa na muongo mmoja uliopita na hiyo ni kengele ya hatari kwa usalama wa kiakili na kisaikolojia wa kizazi cha vijana nchini Uingereza.

Kujiua na kujimalizia maisha ni moja ya sababu kuu za vifo vya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 45 nchini Uingereza na kimsingi idadi ya watu wanaojiunga nchini humo ni kubwa sana ikilinganishwa na ile inayotangazwa na vyombo rasmi vya serikali.