Kuongezeka kwa idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa duniani
(last modified Sat, 16 Sep 2017 13:03:02 GMT )
Sep 16, 2017 13:03 UTC
  • Kuongezeka kwa idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa duniani

Shirika Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza katika ripoti yake mpya kwamba, idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa duniani imeongezeka na kufikia watu milioni 815.

Ripoti hiyo ya FAO imesema kuwa, watu 11 kati ya kila mia moja duniani hawapati chakula cha kutosha. 

Hii ni mara ya kwanza tangu mwanzoni mwa karne hii ya 21 kuwepo ongezeko la idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa duniani. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kiwango cha watu wenye njaa kilikuwa kikipungua lakini kwa mujibu wa ripoti ya FAO sasa idadi hiyo inaongezeka kwa kasi kubwa. Mtaalamu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, Kostas G. Stamoulis anasema: Moja kati ya sababu za kuongezeka idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa duniani ni kupungua kwa kasi ya ustawi wa kiuchumi.

Njaa inahatarisha maisha ya mamilioni ya watu duniani

Ripoti ya pamoja ya FAO, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la Afya Duniani (WHO) na shirika la Mpango wa Chakula duniani (WFP) imesema kuwa, japokuwa ongezeko la joto la dunia si sababu ya moja kwa moja ya umaskini na uhaba wa chakula, lakini joto hilo la dunia pia limechangia katika kuzidisha matatizo yanayohusiana na usalama wa chakula kwa kuzidisha mapigano na majanga ya kimaumbile. Ripoti ya FAO inasema idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa imeongezeko kwa watu milioni 38 katika mwaka wa 2016 na kwamba sababu kuu ya ongezeko la idadi hiyo ya watu wenye njaa ni vita, mapigano na mabadiliko ya hali ya hewa. Ripoti hiyo ya FAO ni tathmini ya kwanza ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa chakula baada ya kuanza utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ambayo moja ya malengo yake muhimu ni kumaliza kabisa njaa duniani ifikapo mwaka 2030.

Kama tulivyotangulia kusema, miongoni mwa sababu kuuza za ongezeko la njaa duniani ni vita, ukatili na ukosefu wa amani. Wahusika wakuu wa machafuko na vita hivyo pia ni nchi tajiri za Magharibi na washirika wao. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni hali ya kusikitisha ya watu zaidi ya milioni 20 wa Yemen. Mamilioni ya wanawake na watoto wa Yemen wamekuwa wahanga wa siasa za kikanda za Saudi Arabia ikiungwa mkono moja kwa moja na madola ya Magharibi yanayodhamini mabomu na silaha zinazotumiwa na utawala wa Aal Saud kuua raia wasio na hatia katika nchi hiyo jirani. 

Watoto wa Yemen, wahanga wa siasa za Saudi Arabia

Ripoti ya FAO pia inaonesha kuwa, kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya njaa na hali ya ukosefu wa amani. Hata hivyo jambo muhimu zaidi katika ripoti hiyo ni kimya cha vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuhusu ripoti hiyo. Vyombo vingi vya habari vya nchi za Magharibi vimepuuza na kunyamazia kimya ripoti hiyo au vimeigusia yaliyomo kwa haraka haraka tu. Hii ni licha ya kwamba, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya FAO, idadi ya watu wanaokabiliwa na tishio la maangamizi kutokana na baa la njaa ni kubwa zaidi kuliko ile ya watu wanaokabiliwa na harakati za kigaidi katika nchi za Magharibi. Si hayo tu bali njaa haina nafasi yoyote katika orodha ya vitisho vya usalama iliyotayarishwa na taasisi na tawala za nchi za Magharibi. Nchi hizo zimesahau au zimejisahaulisha kwamba, njaa na ukosefu wa chakula ndiyo sababu ya ukosefu wa usalama na matatizo mengi ya dunia ya sasa.    

Tags