Russia: Vita na machafuko duniani vinasababishwa na demokrasia chafu ya Marekani
Mkuu wa Baraza la Federesheni ya Russia amesema kuwa, demokrasia ya Marekani ndio chanzo cha machafuko, vita na maafa ya kibinaadamu.
Valentina Ivanovna Matviyenko, ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa kwa mnasaba wa Siku ya Demokrasia ambapo ameonya kwamba, kile kinachozalishwa na Marekani kwa anwani ya 'demokrasia' ni njama tu ya kutaka kulinda satwa yake duniani ambayo inazalisha machafuko, vita na maafa kwa ajili ya nchi nyingine.
Matviyenko ameongeza kuwa, vita mbalimbali vinavyoshuhudiwa duniani, bila shaka yoyote vimesababishwa na uingiliaji wa Marekani katika nchi nyingine. Aidha Mkuu wa Baraza la Federesheni ya Russia amesema kuwa, katika kufikia malengo yao Wamagharibi hutumia njia tofauti za mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi sambamba na kufanya mapinduzi au mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi nyingine, huku wakitoa nara tupu za eti 'Kulindwa Demokrasia.'
Amesisitiza kuwa, hii leo hakuna mtu ambaye yuko tayari kuhadaika na kaulimbiu hizo za Wamagharibi. Ameweka wazi kwamba, hakuna nchi au kundi lolote duniani ambalo lina haki ya kudai kuwa lina demokrasia bora zaidi na hivyo kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano wake.