Nchi tano muhimu za Ulaya zampinga Trump kuhusu JCPOA
Maafisa waandamizi wa nchi tano za Ulaya wamesisitiza kuwa nchi zao zitaendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwani ni makubaliano ya kimataifa kama ambavyo wamesisitiza pia kuwa nchi zao zitaendelesha kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga tofauti.
Mabalozi wa nchi tano za Uingereza, Ubelgiji, Denmark, Poland na Uholanzi walisema jana Jumatano kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni makubaliano ya kimataifa na kwamba pande zote zinazohusika kwenye makubaliano hayo zinapaswa kuyaheshimu. Makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Marekani, maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016. Hata hivyo hadi hivi sasa serikali ya Marekani imekuwa ikivikanyaga wazi wazi na kwa makusudi vipengee vya makubaliano hayo huku Iran ikiwa imeyaheshimu kikamilifu.
Nicholas Hopton, balozi wa Uingereza mjini Tehran amesema katika baraza la ushirikiano wa Iran na Ulaya kwamba, London itaendelea kuheshimu makubaliano hayo ya kimataifa na itaendelea kufanya mashauriano kuhusu udharura wa kuyaheshimu.
Baraza la ushirikiano wa Iran na Ulaya kwa kifupi EIF liliundwa miaka minne iliyopita kwa lengo la kutia nguvu udiplomasia wa kibiashara baina ya Iran na Magharibi.
Baraza hilo limekuwa likitoa fursa muhimu za kubadilishana taarifa na mawasiliano baina ya pande mbili hususan katika nyuga za kibiashara na viwanda.