Ujerumaini, Uingereza, Ufaransa: Tutahakikisha makubaliano ya JCPOA yanalindwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuwa nchi yake pamoja na Uingereza na Ufaransa zina mtazamo mmoja kuhusiana na wajibu wa kulindwa na kuheshimiwa mapatano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la JCPOA.
Sigmar Gabriel alisema hayo jana (Jumatatu) na kuongeza kuwa, yeye pamoja na Boris Johnson na Jean-Yves Le Drian, mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Uingereza na Ufaransa na vile vile Federica Mogherini, mkuu wa siasa za kigeni za Umoja wa Ulaya wana kauli na mtazamo mmoja kuhusu udharura wa kulindwa na kuheshimiwa mapatano hayo ya nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema hayo baada ya kufanyika mazungumzo ya mawaziri hao watatu na mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa, kulindwa mapatano ya nyuklia kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran ni kwa manufaa ya pande zote.
Itakumbukuwa kuwa tarehe 13 mwezi uliopita wa Oktoba, 2017, Rais wa Marekani, Donald Trump alidai kuwa mapatano ya JCPOA ni kama zimwi na kutishia kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo.
Hata hivyo msimamo huo wa Trump ulipingwa vikali na waitifaki wa Marekani barani Ulaya na kumlazimisha alegeze msimamo kwa muda.