Kuendelea hatua za uhasama za Marekani dhidi ya Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38637-kuendelea_hatua_za_uhasama_za_marekani_dhidi_ya_venezuela
Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amekosoa vikali kuendelea siasa za uhasama za serikali ya Marekani dhidi ya nchi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 07, 2018 09:20 UTC
  • Kuendelea hatua za uhasama za Marekani dhidi ya Venezuela

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amekosoa vikali kuendelea siasa za uhasama za serikali ya Marekani dhidi ya nchi yake.

Rais Maduro aliyasema hayo Ijumaa kupitia ripoti iliyozungumzia harakati za vyombo vya habari vya Marekani dhidi ya Venezuela na kusema: Mwaka 2017 vyombo vya habari vya Marekani vilitoa habari zaidi ya 3880 dhidi ya serikali ya Caracas. Hatua hiyo imetajwa na Rais Maduro kuwa sawa na kuzusha vita dhidi ya Venezuela na serikali ya nchi hiyo. Kati ya vyombo vya habari vya Marekani, shirika la Bloomberg linashika nafasi ya kwanza kwa kuivunjia heshima serikali na watu wa nchi hiyo. Baada ya shirika hilo, yanafuatia mashirika ya Herald Tribune na Washington Post ambayo ni maarufu kwa kueneza propaganda dhidi ya serikali ya Caracas. Kwa mujibu wa Rais Maduro mashirika kadhaa ya Uingereza yenye makao yake nchini Marekani kama vile Shirika la Habari la Reuters na Associated Press nayo yamekuwa yakieneza uongo dhidi ya serikali ya Venezuela.

Trump, rais wa Marekani

Aidha mbali na vita vya propaganda, serikali ya Marekani imekuwa ikitekeleza vikwazo dhidi ya viongozi wa serikali na uchumi wa taifa hilo. Katika uwanja huo, siku ya Ijumaa Wizara ya Fedha ya Marekani iliwawekea vikwazo viongozi wanne wengine wa kijeshi wa Venezuela kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na ukandamizaji. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, fedha za viongozi hao zilizopo Marekani zitazuiliwa na hakuna raia yeyote wa Marekani atakayeruhusiwa kufanya muamala wowote na watu hao. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, hatua ya Trump kuzidi kuisakama Venezuela inaonyesha kwamba serikali ya Caracas imekuwa kizingiti muhimu katika njia ya kujitanua Marekani katika eneo la Amerika ya Latini. Ukweli ni kwamba tangu Trump alipoingia White House, amefuata mkondo tofauti kuhusiana na maeneo mengi ya dunia ikiwemo Amerika ya Latini kinyume na mtangulizi wake Barack Obama. Katika uongozi wake, Obama alikuwa akitumia nguvu lakini kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa ibara nyingine ni kwamba, msingi na siasa za Trump na Obama ni moja lakini zinatofautiana katika utekelezaji wake.

Bendera ya Venezuela

Aidha Obama alikuwa akijitahidi kutumia udiplomasia na kuukinaisha upande wa pili kukubali siasa za Marekani. Kinyume chake, mfumo wa Trump umejengeka juu ya mabavu. Vitisho vya kutekeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Venezuela, ongezeko la vikwazo na matamshi  ya vitisho dhidi ya serikali ya nchi hiyo, yote hayo yanabainisha mwenendo mpya wa serikali ya Washington dhidi ya serikali ya Caracas. Kiujumla ni kwamba, Rais Donald Trump ameamua kufuata siasa za uhasama dhidi ya Amerika ya Latini ambapo hata mpango wa kujenga ukuta wa kibaguzi katika mpaka wake na Mexico umetafsiriwa na raia wa mataifa ya ukanda huo kuwa ni hatua ya udhalilishaji.

Dilma Rousseff, rais wa zamani wa Brazil

Katika uwanja huo Dilma Rousseff, rais wa zamani wa Brazil amekumbusha matamshi yaliyowahi kutolewa na Trump kuhusu waandamanaji wa upinzani nchini Venezuela kwamba, wanatetea demokrasia, siasa ambazo pia zilitekelezwa na Washington katika kuwaunga mkono wapinzani nchini Syria. Siasa hizo za kimaslahi na kichochezi za Marekani hatimaye zilipelekea kubuniwa kundi hatari la kigaidi la Daesh ambalo halina mfungamano wowote na demokrasia inayodaiwa kutetewa na Marekani. Kwa vyovyote vile inaonekana kuwa uhasama wa Marekani hautafanikiwa kuidhoofisha serikali kuu ya Caracas na hata huenda ukaimarisha umoja wa kitaifa wa nchi hiyo dhidi ya uingiliaji wa kigeni.