Mogherini: Umoja wa Ulaya utaendelea kuheshimu maafikiano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38839-mogherini_umoja_wa_ulaya_utaendelea_kuheshimu_maafikiano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, umoja huo umeamua kuheshimu maafikiano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2018 12:56 UTC
  • Mogherini:  Umoja wa Ulaya utaendelea kuheshimu maafikiano ya nyuklia ya JCPOA

Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, umoja huo umeamua kuheshimu maafikiano ya nyuklia ya JCPOA.

Federica Mogherini amesema hayo katika kikao cha kujadili maafikiano hayo kilichofanyika mjini Brussels Ubelgiji na kuongeza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ripoti tisa zinazothibitisha kuwa Iran imeheshimu vipengee vya maafikiano hayo na kuthibitisha pia kuwa miradi ya nyuklia ya Iran ni ya amani kikamilifu suala ambalo Umoja wa Ulaya nao umeweza kulithibitisha pia kupitia timu ya pamoja ya JCPOA.

Mkutano wa Iran na nchi za Ulaya katika makao makuu ya EU mjini Brussels, Ubelgiji

 

Aidha amesisitiza kuwa, JCPOA ni maafikiano ya kimataifa yaliyofikiwa baina ya mataifa kadhaa na ni kitu cha dharura kwa usalama wa Ulaya na eneo la Mashariki ya Kati. Ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya umekusudia kuyalinda kikamilifu maafikiano hayo yakiwa ni wenzo mkuu wa kuzuia uenezaji na uzalishaji wa silaha za nyuklia.

Vile vile amesema, Umoja wa Ulaya unataka maafikiano ya JCPOA yalindwe kwani yameleta matunda mazuri na yameifanya dunia kuwa na amani zaidi hivyo unazitaka pande zote ziyaheshimu na kuyatekeleza kikamilifu maafikiano hayo.

Itakumbukwa kuwa leo (Alkhamisi) kumefanyika kikao maalumu katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonana katika kikao hicho na Federika Mogherini, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumaini, Uingereza na Ufaransa na kujadiliana nao hali ya karibuni kabisa ya maafikiano ya nyuklia ya JCPOA.