Amnesty yataka kufanyike uchunguzi wa mauaji ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43186-amnesty_yataka_kufanyike_uchunguzi_wa_mauaji_ya_wapalestina
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kukomeshwa ukandamizaji unaofanywa na maafisa wa utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wa Palestina na kuanzishwa uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na askari wa utawala huo dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2018 09:50 UTC
  • Amnesty yataka kufanyike uchunguzi wa mauaji ya Wapalestina

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kukomeshwa ukandamizaji unaofanywa na maafisa wa utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wa Palestina na kuanzishwa uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na askari wa utawala huo dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina.

Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa, katika wiki tatu zilizopita dunia imeshuhudia utumiaji wa nguvu kupita kiasi na mauaji ya askari wa Israel dhidi ya waandamanaji wakiwemo watoto ambao dhambi yao ni kutaka kukomeshwa siasa za kidhalimu za Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kuishi kwa heshima.

Magdalena Mughrabi ameongeza kuwa, maafisa wa Israel wanapaswa kukomesha sera hizo za mauaji haraka iwezekanavyo na kuheshimu sheria za kimataifa.

Wapalestina wasiopungua 40 wakiwemo watoto wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel, Gaza

Afisa huyo wa Amnesty International amesisitiza kuwa, utumiaji mkubwa wa silaha dhidi ya waandamanaji wa Palestina na kuwaua unapaswa kuchunguzwa.

Wananchi wa Ukanda wa Gaza huko Palestina tangu tarehe 30 Machi sambamba na maadhimisho ya Siku ya Ardhi wamekuwa wakifanya maandamano makubwa yaliyopewa jina la Haki ya Kurejea. Maandamano hayo yamekabiliwa na ukatili wa askari wa utawala haramu wa Israel ambao hadi sasa wameua raia wasiopungua 40.