Indhari ya Ufaransa juu ya kutokea vita vya ndani barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43360-indhari_ya_ufaransa_juu_ya_kutokea_vita_vya_ndani_barani_ulaya
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amehutubia bunge la Ulaya na kutoa indhari juu ya kutokea vita vya ndani barani humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2018 21:09 UTC
  • Indhari ya Ufaransa juu ya kutokea vita vya ndani barani Ulaya

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amehutubia bunge la Ulaya na kutoa indhari juu ya kutokea vita vya ndani barani humo.

Akiashiria kwamba hivi sasa viongozi wa Ulaya wana majukumu makubwa kuliko wakati wowote ule, Macron ameonya juu ya kuwepo tofauti kubwa na wasi wasi ndani ya nchi za Ulaya na kwamba, kujivunia utaifa kumegubika umoja katika bara hilo. Hotuba ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa imetolewa katika hali ambayo, kabla ya hapo pia baadhi ya viongozi wa Ulaya walionya juu ya kushtadi tofauti za kimtazamo kati ya nchi za Ulaya. Viongozi wa Umoja wa Ulaya hususan katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, wamekuwa wakivutana kwa masuala tofauti likiwemo suala la Brexit na namna ya kujiondoa serikali ya Uingereza katika Umoja wa Ulaya, suala la wahajiri na wakimbizi na namna ya kuwapokea watu hao, mvutano wa mipaka ya ndani na kutoshirikishwa baadhi ya nchi katika maamuzi makubwa na pia kutekelezwa baadhi ya maamuzi ya kiuchumi yakiwemo masuala ya mfumo wa uratibu wa kodi. Katika uwanja huo, Rais Andrzej Duda wa Poland amesema:

Rais Andrzej Duda wa Poland

"Ikiwa Brussels itaendelea na mwenendo wake wa sasa, itapelekea kuusambaratisha Umoja wa Ulaya." Tofauti hizo za kimtazamo ndizo zimepelekea hata baadhi ya weledi wa mambo kuonya juu uwezekano wa kuchukuliwa madaraka ya mataifa wa Ulaya na mirengo ya kitaifa na vyama vya mrengo wa kulia vyenye siasa kali kwa anuani ya wapinzani wakuu wa siasa za sasa barani humo, za kuwa na mielekeo ya pamoja kieneo. Kama ilivyoshuhudiwa miaka ya hivi karibuni katika mataifa kama Ujerumani, Austria, Italia na Jamhuri ya Czech, ambapo vyama vya mrengo wa kulia na vyenye kuchupa mipaka vimeweza kupata ushindi wa kiwango fulani katika chaguzi za bunge ndani ya mataifa hayo.

Miongoni mwa matatizo yanayoukabili Umoja wa Ulaya

Suala hilo pamoja na mambo mengine linatajwa kuwa ni kengele ya hatari kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya na pia kwa nara na malengo makuu ya kuwa na mielekeo ya pamoja ya viongozi hao. Aidha suala hilo limekuwa na umuhimu kiasi kwamba, iwapo vyama na mirengo hiyo itapata nguvu katika jamii za Ulaya sambamba na kuendelea kupata ushindi wa kisiasa na kuvutia uungaji mkono wa kijamii, vitaweza kubadili njia ya ushirikiano wa Ulaya na kuzielekeza kwenye ombwe kubwa. Hayo yanajiri katika hali ambayo kwa mujibu wa weledi wa mambo, kuchukuliwa maamuzi kama vile kuwagawa wahajiri, kuwekwa mfumo wa kodi wa namna moja bila kuzingatia mazingira ya nchi husika, kushtadi matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira katika nchi nyingi za umoja huo, suala la kujiondoa Uingereza katika umoja huo (Brexit) na kadhalika kurefushwa mazungumzo kati ya nchi wanachama, ni mambo yaliyopelekea kuongezeka kiwango cha manung'uniko ndani ya Umoja wa Ulaya.

Suala la wahijiri pia linachangia mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya

Mkabala wa kujiondoa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Euro, kutaka zitumie sarafu zao za taifa, kuongezeka mielekeo ya kutegemea zaidi uwezo wa ndani wa kiuchumi, namna ya kuamiliana na wahajiri pamoja na kuweka sheria kali kuhusiana na suala hilo, ni miongoni mwa mapendekezo ya baadhi ya nchi za eneo hilo na nara za vyama vya mrengo wa kulia vinavyoendesha harakati zao barani Ulaya. Kuhusiana na suala hilo, Jacek Czaputowicz Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland amesema: "Ongezeko la wimbi la upinzani dhidi ya muelekeo wa ushirikiano wa pamoja barani Ulaya, halisababishwi na udhaifu wa demokrasia ndani ya EU, bali ni matokeo ya jambo hilo." 

Jacek Czaputowicz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland

Alaakullihal, indhari ya kutokea vita vya ndani barani Ulaya imetolewa na viongozi wa EU, katika hali ambayo, kuzidi kupata nguvu mielekeo ya utengano, kunakinzana waziwazi na falsafa ya kuwepo Umoja wa Ulaya uliojengwa juu ya msingi wa kuwa na ushirikiano na muelekeo wa pamoja wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi wanachama. Na hii ni katika hali ambayo Umoja wa Ulaya unakabiliwa na changamoto nyingi za kieneo, likiwemo suala la kuboresha mahusiano na Marekani hasa kwa kuzingatia siasa za Rais Donald Trump wa nchi hiyo na kadhalika changamoto kuhusiana na Russia kwa kuzingatia mgogoro wa Ukraine na pia mustakbali wa mahusiano kati ya Moscow na EU hususan katika uga wa uingizaji gesi kutoka Russia.