Wahajiri wa Nigeria waishtaki Italia kwa kukanyaga haki zao
Kundi la wahajiri raia wa Nigeria ambao ni manusura wa ajali za boti zilizoshuhudiwa mwaka jana wameifungulia mashitaka serikali ya Italia kwa kukiuka haki zao za binadamu.
Violeta Moreno-Lax, mshauri wa masuala ya sheria wa shirika la Global Legal Action Network amewaambia waandishi wa habari kuwa, wahajiri hao wapatao 17 kwa usaidizi wa mawakili wanne wamewasilisha faili la kesi hiyo katika Mahakama ya Haki ya Ulaya.
Manusura hao wanaituhumu serikali ya Italia kukiuka haki zao kwa kushirikiana na Gadi ya Pwani ya Libya kwa kurejesha boti za wahajiri hao kwa nguvu kaskazini mwa Afrika.
Wahajiri hao wa Nigeria wanasema Italia ilikanyaga vipengee kadhaa vya Hati ya Ulaya kuhusu Haki za Binadamu, vikiwemo vinavyopiga marufuku watu kukandamizwa, kufanywa watumwa, au maisha yao kuwekwa hatarini.

Umoja wa Mataifa, mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyombo vya habari vimesema kuwa wahajiri hao wa Kiafrika walikabiliwa na mazito hayo matatu wakati wakirejeshwa kwa nguvu kaskazini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM), wahajiri wapatao 90 waliaga dunia katika maji ya pwani ya Libya baada ya boti yao kuzama baharini Februari mwaka huu.