Wafungwa Waislamu Marekani wanyimwa chakula, walazimishwa kula nyama ya nguruwe
(last modified Thu, 24 May 2018 14:38:38 GMT )
May 24, 2018 14:38 UTC
  • Wafungwa Waislamu Marekani wanyimwa chakula, walazimishwa kula nyama ya nguruwe

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limewasilisha faili la kesi mahakamani kuwashtaki maafisa wa Idara ya Magereza ya Alaska, kwa kuwanyima chakula wafungwa Waislamu mbali na kuwalazimisha kula nyama ya nguruwe katika mwezi huu wa Ramadhani.

Lena Masri, Mkurugenzi wa CAIR katika masuala ya sheria amesema anatumai mahakama ya jimbo la Alaska itawawajibisha wahusika wa vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria, dhidi ya wafungwa Waislamu katika Gereza la Anchorage jimboni hapo.

Baraza hilo linaitaka mahakama itoe agizo la kutaka maafisa wa gereza hilo wawape chakula wafungwa hao Waislamu na kisichanganywe na nyama, mafuta au bidhaa zinazotokana na nguruwe.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani limesema baadhi ya wafungwa hao Waislamu wanapewa vyakula baridi, vilivyo na kiwango cha chini cha virutubisho na visivyolika na hivyo baadhi yao wanashindwa kuvila kabisa, licha ya kushinda mchana kutwa na saumu.

CAIR imesema wafungwa hao wa Kiislamu wanabaguliwa kwa misingi ya dini yao na wanalazimishwa kula vyakula ambavyo vimeharamishwa na dini yao jambo ambalo sio tu linakiuka haki zao za msingi kama wafungwa bali pia linahujumu dini yao.

Maafisa wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani

Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili mwaka huu, utafiti uliofanywa na shirika la kutetea haki za binadamu nchini Marekani la Institute for Social Policy and Understanding (ISPU) ulibainisha kuwa, watuhumiwa wa uhalifu Waislamu au wenye majina ya Kiislamu nchini Marekani wanahukumiwa vifungo virefu zaidi, na habari hizo kuvaliwa njuga na vyombo vya habari, kuliko watuhumiwa wasiokuwa Waislamu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, iwapo mshukiwa Muislamu na asiyekuwa Muislamu watakamatwa kwa tuhuma za kula njama ya kutekeleza shambulizi la bomu, Muislamu atahukumiwa kifungo kizito cha hadi miaka 20 jela huku asiyekuwa Muislamu akifungwa miaka mitano jela.