Umoja wa Ulaya hautambui rasmi kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina
Msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo hautambui rasmi hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kukali kwa mabavu ardhi za Wapalestina ulizoziteka mwaka 1967.
Kwa mujibu wa televisheni ya Russia Today, Maya Kosyanchych, msemaji wa Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ambaye alikuwa akizungumzia hatua ya hivi karibuni ya seneti ya Ireland ya kupasisha mswada wa kususia bidhaa zote zinazotengenezwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, amesema kuwa umoja huo pia utafuatilia mkondo wa sheria hiyo mpya ya Ireland. Siku ya Jumatano, seneti ya Ireland ilipasisha kwa wingi wa kura, mswada unaonuia kupiga marufuku kuingizwa nchini humo bidhaa zinazotengenezwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwa ni katika hatua yake ya kuunga mkono taifa la Palestina kutokana na uporaji wa ardhi zake unaofanywa na utawala haramu wa Israel. Hatua hiyo ya kijasiri ya seneti ya Ireland imeukasirisha sana utawala huo haramu.
Licha ya kuwepo maazimio chungu nzima ya Umoja wa Mataifa yanayopinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoporwa za Wapalestina, lakini utawala ghasibu wa Israel umeyapuuza maazinio hayo yote na kuendelea na ujezi wa vitongoji katika ardhi hizo kutokana na uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani. Katika miaka ya hivi karibuni taasisi za kiraia na jumuiya za wanachuo wa Ulaya na Marekani zimeanzisha harakati kubwa za kupiga marufuku na kususia bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni wanaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.