Jul 26, 2018 07:41 UTC
  • Unicef: Katika kila dakika 3, binti mmoja anaambukizwa virusi vya HIV

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umesema mabinti na wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na 19 wanajenga thuluthi mbili ya watu walioambukizwa virusi hatari vya HIV mwaka jana 2017.

Akihutubu katika Duru ya 22 ya Kongamano la Ukimwi jana Jumatano mjini Amsterdam, Uholanzi, Henrietta Fore, Mkuu wa Unicef amesema kwa kila dakika tatu, binti mmoja barobaro huambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Amesema katika aghalabu ya nchi, mabinti wanaoambukizwa virusi hivyo ni wale waliotengwa au kutelekezwa na jamii na familia, baadhi yao wakiwa katika hatari ya maambukizi kutokana na udhaifu wao ama wa kisaiolojia au kimwili.

Takwimu hizo za Unicef zinaonesha kuwa, vijana 130,000 chini ya miaka 19 waliaga dunia kutoka na Ukimwi mwaka jana, huku maambukizi mapya 430,000 yakiripotiwa, sawa na watu 50 kwa kila saa moja. 

Aidha watu milioni 35 wamepoteza maisha tangu virusi vya HIV na Ukimwi ulipoenea duniani katika miaka ya 1980. 

Wiki iliyopita, shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) lilitangaza kuwa, maambukizi ya virusi vya Ukimwi yameongezeka katika mataifa 50 duniani na kwamba watu wapya wanaombukizwa virusi hivyo, hawapati dawa za kuwasaidia kuishi muda mrefu. 

Inakadiriwa kuwa, watu milioni 37 wanaishi na virusi vya Ukimwi HIV duniani, huku bara la Afrika likiwa na maambukizi mengi zaidi.

Tags