Indonesia yalivunja kundi kubwa lenye mahusiano na magaidi wa Daesh
Mahakama ya Indonesia imevunja kundi kubwa 'Jamaatu-Nashratu-Daulah' lenye mafungamano na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kwa tuhuma za kuendesha harakati za kigaidi ndani ya nchi hiyo.
Kundi la Jamaatu-Nashratu-Daulah' kwa kifupi 'JAD' lilikuwa likiongozwa na Aman Abdur-Rahman, ambaye mwezi uliopita alihukumiwa kunyongwa kwa kuratibu vitendo vya kigaidi nchini humo. Miongoni mwa harakati za kigaidi zilizotekelezwa na kundi hilo hatari, ni pamoja na hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa mwezi Mei mwaka huu dhidi ya mji wa Surabaya, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Indonesia.
Katika shambulizi hilo ambalo liliyalenga makanisa matatu mjini hapo, watu 11 waliuawa na wengine 40 walijeruhiwa. Inafaa kuashiria kuwa, vijana wengi wa Indonesia walijiunga na kundi la Daesh, baada ya kuibuka mzozo nchini Syria na Iraq, hasa kutokana na propaganda zilizokuwa zikienezwa na genge hilo linaloungwa mkono na Marekani, Israel, Saudia na baadhi ya nchi nyingine.