Korea Kaskazini yalalamikia undumakuwili wa Marekani katika uga wa nyuklia
Serikali ya Korea Kaskazini kupitia gazeti la chama tawala la Rodong Sinmun, imesema kuwa, hatua ya kurefushwa mkataba wa nyuklia kati ya Marekani na Japan ni kitendo kilicho 'dhidi ya ubinaadamu na dhidi ya amani.'
Kwa mujibu wa gazeti hilo serikali ya Pyongyang sambamba na kukosoa ushirikiano wa kinyuklia uliopo kati ya Marekani na Japan katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, imesisitiza kuwa, Washington imekuwa na mienendo ya kindumakuwili kuhusu Korea Kaskazini na Japan katika uga wa masuala ya nyuklia. Gazeti hilo limefafanua kuwa, katika hali ambayo Marekani imeiwekea mashinikizo Pyongyang kutokana na masuala ya nyuklia, lakini wakati huo huo inashirikiana na Japan katika uga huo.
Gazeti la Rodong Sinmun limeongeza kwamba, wakati ambao Marekani iliipatia haki ya kuzalisha nishati ya nyuklia mwaka 1988, Tokyo iliongeza hazina yake ya kemikali ya Plutonium kiasi kwamba, jumla ya tani 47 za kemikali kati ya tani 518 za mada hiyo zilizopo duniani kote zilihifadhiwa na nchi hiyo. Kwa mujibu wa gazeti hilo, kiwango hicho kinaweza kuzalisha mabomu 800 ya nyuklia huko Japan pekee. Mkataba wa nyuklia kati ya Marekani na Japan uliotiwa saini mwaka 1988 kwa kipindi cha miaka 30 ulimalizika hivi karibuni. Hata hivyo baada ya kufanyika mazungumzo kati ya pande mbili, umerefushwa tena.