Trump na Shinzo Abe: Tutaendelea kuibana kwa vikwazo Pyongyang
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47651-trump_na_shinzo_abe_tutaendelea_kuibana_kwa_vikwazo_pyongyang
Rais Donald Trump wa Marekani na Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Japan wamesema kuwa, wataendeleza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini ili kutatuliwa kadhia ya silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.
(last modified 2025-11-05T05:46:17+00:00 )
Aug 24, 2018 07:56 UTC
  • Trump na Shinzo Abe: Tutaendelea kuibana kwa vikwazo Pyongyang

Rais Donald Trump wa Marekani na Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Japan wamesema kuwa, wataendeleza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini ili kutatuliwa kadhia ya silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.

Viongozi hao wameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na kutangaza kwamba wataendeleza ushirikiano katika uga wa vikwazo dhidi ya Pyongyang.

Mazungumzo hayo yamefanyika kabla ya safari ya nne ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mjini Pyongyang. Washington inafanya juhudi za kutaka kuishawishi Korea Kaskazini ili ikubali kupiga hatua muhimu katika njia ya kutokomeza silaha zake za nyuklia. Kabala ya hapo, Shinzo Abe alinukuliwa akisema kuwa, Trump ameahidi kuisadia Japan katika suala la kurejeshwa raia wa nchi hiyo waliotekwa nyara katika muongo wa 70 na 80.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini

Abe analitambua suala hilo kuwa kipaumbele cha kwanza kwa serikali ya Tokyo. Katika fremu hiyo, Japan ilmetangaza utayarifu wake kwa ajili ya kushirikiana na Marekani, Korea Kusini, China na Russia kwa ajili ya kuangamiza miradi ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya Korea Kaskazini sambamba na kutatuliwa suala la raia wake waliotekwa nyara.

Mashinikizo na vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, vinajiri katika hali ambayo Trump na Kim Jong-un, walikutana nchini Singapore tarehe 12 Juni mwaka huu na kutiliana saini makubaliano kadhaa kwa ajili ya kuboresha mahusiano ya nchi mbili.