Hamu ya Korea Kaskazini kuboresha uhusiano wake na Japan
(last modified Tue, 28 Aug 2018 07:56:04 GMT )
Aug 28, 2018 07:56 UTC
  • Hamu ya Korea Kaskazini kuboresha uhusiano wake na Japan

Mwanzoni mwa mwezi huu, Korea Kaskazini ilimuachilia huru raia wa Japan aliyekamatwa na nchi hiyo kwa tuhuma za kufanya ujasusi.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini sambamba na kuthibitisha habari ya kuachiliwa huru raia huyo wa Japan kwa jina la Tomoyuki Sugimoto, limetangaza kwamba, viongozi wa Pyongyang wamefumbia macho makosa yake na kuamua kumuchilia huru kwa misingi ya kibinaadamu. Kabla ya hapo vyombo vya habari vya Japan vilitangaza kwamba, Sugimoto ambaye ni mpiga picha raia wa Japan, alifanya safari nchini Korea Kaskazini na kampuni moja ya kigeni ya utalii, hata hivyo baadaye akakamatwa na serikali ya Pyongyang kwa tuhuma za kupiga picha na kufanya ujasusi kwenye taasisi za kijeshi za nchi hiyo. Kabla ya hapo serikali ya Korea Kaskazini ilitangaza kwamba, ilikuwa inamshikilia Sugimoto kwa ajili ya kumuhoji zaidi kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zinamkabili kuhusu uvunjaji wa sheria za nchi hiyo.

Tomoyuki Sugimoto, raia wa Japan aliyekuwa anatuhumiwa na Pyongyang kwa ujasusi

Hatua hiyo ya Pyongyang inaonyesha nia yake njema kwa ajili ya kuboresha uhusiano na serikali ya Japan. Baada ya kuanza mazungumzo kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini mwezi Februari mwaka huu, viongozi wa Pyongyang na katika fremu ya siasa za kutatua mizozo na baadhi ya nchi za eneo, iliamua kupunguza tofauti zake na Japan. Kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, stratijia ya kutatua mzozo na mivutano ya muda mrefu na Korea Kusini, inahitajia kufutwa sababu zinazoibua suitafahamu katika Rasi ya Korea. Katika orodha ya sababu hizo ni kuchochewa mizozo inayotokana na pande zilizo nje ya eneo zikiwemo siasa za uchochezi za Marekani katika eneo hilo. Ni kwa msingi huo, ndio maana viongozi wa Pyongyang wakataka kusimamishwa maneva ya Marekani na Korea kaskazini pamoja na nchi nyingine za eneo, ikiwemo Japan katika eneo la mashariki mwa Asia.

Uhusiano wa Korea Kaskazini na Japan, umekuwa ukivurugwa na Marekani kwa lengo la kuuza silaha

Mbali na hayo ni kwamba, Kiongozi wa Korea Kaskazini anaamini kwamba, juhudi za utatuzi wa mzozo kati yake na Korea Kusini kwa ajili ya kuimarisha usalama katika eneo, bado hazitoshi na ni lazima mzozo wa Pyongyang na Tokyo uendelee kupungua kupitia mwenendo wa mazungumzo kati ya Korea mbili. Kuhusu hilo, hatua ya Marekani ya kupiga ngoma ya kuifanya Pyongyang ichukiwe na kuogopwa na nchi za eneo ikiwemo Japan, inatajwa kuwa kuzuizi kikuu katika mwenendo wa kupunguza mzozo wa Korea Kaskazini na Japan. Hii ni kusema kuwa, White House inafanya juhudi kubwa kueneza uchochezi katika eneo la Peninsula ya Korea ili iweze kuuza silaha na zana nyingine za kijeshi kwa nchi za eneo hilo. Katika mazingira hayo, Korea Kaskazini mbali na kuchukua hatua chanya mkabala na kadhia ya kutatuliwa mzozo kati yake na Japan, sambamba na kumuachilia huru raia wa nchi hiyo aliyekuwa anashikiliwa kwa tuhuma za ujasusi nchini humo, imeonyesha nia yake njema kwa ajili ya kuanza mazungumzo kati ya pande mbili kwa lengo la kupunguza tofauti zao.

Korea Kaskazini imeonyesha nia njema na nchi jirani

Katika kukabiliana na stratijia hiyo ya Korea Kaskazini, Japan na kinyume na Korea Kusini bado imeendelea kutilia shaka mwenendo wa mazungumzo kati ya Pyongyang na Korea Kusini pamoja na Marekani na katika uwanja huo, mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kushadidishwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo kwa lengo la kuhitimishwa miradi ya nyuklia na makombora yake ya balestiki. Kuhusiana na suala hilo, Air Ching Ying, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Nchi tofauti ikiwemo Japan zinatakiwa sambamba na kuzingatia maslahi yao ya kiusalama, zitilie maanani wasi wasi wa usalama wa nchi nyingine, kama ambavyo kustawishwa ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili kati ya Japan na Marekani hakutakiwi kuwa na madhara kwa maslahi ya upande wa tatu katika eneo." Mwisho wa kunukuu. Alaa kullihal, Korea Kaskazini inataraji kwamba serikali ya Japan,  kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa sambamba na kudiriki hali ya sasa ya eneo la Korea, itaandaa uwanja wa kupunguza mzozo katika uhusiano wa nchi mbili.

Tags