Umoja wa Ulaya wataka Israel isitishe kubomoa nyumba za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47981-umoja_wa_ulaya_wataka_israel_isitishe_kubomoa_nyumba_za_wapalestina
Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametoa mwito kwa utawala wa Kizayuni wa Israel usitisha mara moja bomoa bomoa ya nyumba za Wapalestina.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 08, 2018 10:56 UTC
  • Umoja wa Ulaya wataka Israel isitishe kubomoa nyumba za Wapalestina

Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametoa mwito kwa utawala wa Kizayuni wa Israel usitisha mara moja bomoa bomoa ya nyumba za Wapalestina.

Katika taarifa yake ya leo Jumamosi, Mogherini ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe kubomoa kijiji cha Wapalestina cha Khan al-Ahmar, mashariki mwa Quds Tukufu (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.

Mogherini amesema mahakama moja ya utawala wa Kizayuni wa Israel imekataa maombi ya wakaazi wa kijiji cha Khan al-Ahmar na kuamuru kibomolewe.

Aidha amesema Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo zimekuwa zikisisitiza kwa muda mrefu kuwa, sera za Israel za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni kinyume cha sheria za kimataifa kama ambavyo pia ni kinyume cha sheria kubomoa nyumba za Wapalestina na kuwafukuza katika makazi yao ya jadi.

Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini

Amesema bomoabomoa hiyo ya nyumba za Wapalestina itapelekea watu wengi kukosa makazi, wakiwemo watoto na hivyo kuhatarisha juhudi za kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Kijiji cha Khan al-Ahmar ni cha Wapalestina wa jamii ya Badawi na kiko katika jangwa la Negev na wakaazi wa kijiji hicho walifukuzwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kutoka ardhi zao za jadi mwaka 1953 na kulazimishwa kuhamia eneo wanaloishi hivi sasa ambalo nalo mahakama imeamuru wafukuzwe.

Pambizoni mwa kijiji cha Khan al-Ahmar kuna vitongoji kadhaa vya walowezi wa Kizayuni na hivyo utawala wa Kizayuni unataka kubomoa kijiji hicho na mahala pake kujenga vitongoji vya walowezi wao kinyume cha sheria za kimataifa.