Wafuasi wa Ahlul-Bayti duniani wakumbuka mauaji ya Imam Hussein (as)
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48274-wafuasi_wa_ahlul_bayti_duniani_wakumbuka_mauaji_ya_imam_hussein_(as)
Waislamu wapenzi wa familia ya Mtume Muhammad (saw) katika nchi mbalimbali za dunia leo wameshiriki maombolezo ya siku ya Ashura, ambayo aliuawa shahidi ndani yake mjukuu wa Mtume, yaani al-Imam Hussein bin Ali (as).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2018 11:27 UTC
  • Wafuasi wa Ahlul-Bayti duniani wakumbuka mauaji ya Imam Hussein (as)

Waislamu wapenzi wa familia ya Mtume Muhammad (saw) katika nchi mbalimbali za dunia leo wameshiriki maombolezo ya siku ya Ashura, ambayo aliuawa shahidi ndani yake mjukuu wa Mtume, yaani al-Imam Hussein bin Ali (as).

Katika maombolezo hayo, Waislamu wa miji yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshiriki kwa wingi Swala ya Adhuhuri ya mchana wa siku ya Ashura, wakienzi na kukumbuka Swala ya mwisho ya mjukuu huyo wa Mtume kabla ya kuuawa shahidi yeye pamoja na watu wa familia ya Nabii huyo wa Allah na pia masahaba wake wema mwaka 61 Hijiria.

Maombolezo kama hayo pia yamefanyika katika nchi nyingi za dunia kama Iraq, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, Syria, Lebanon, Azerbaijan, China, mataifa mbalimbali ya Ulaya, Marekani na Afrika. Katika nchi za Afrika Mashariki kama Tanzania mbali na wafuasi wa Ahlul-Bayti wa Mtume kushiriki matembezi ya usiku wa kuamkia siku ya Ashura, pia walishiriki harakati mbalimbali za kijamii na kibinadamu ikiwemo kugawa maji, kujitolea damu na kufanya usafi katika kumuenzi Imam Hussein (as).

Waislamu wakishiriki swala ya adhuhuri ya siku ya Ashura

Harakati za tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Mtume zimekuwa zikiibua hisia za Waislamu na wasio Waislamu kote duniani kutokana na dhulma iliofanyiwa familia ya Mtume wa Uislamu, makumi ya karne zilizopita. Jumla ya watu 72 waliokuwa pamoja na Imam Hussein (as) waliuawa shahidi kinyama baada ya kupambana kishujaa na maelfu ya askari wa mtawala Yazid mwana wa Muawiya, ambapo baada ya mauaji, vichwa vyao vilitenganishwa na viwiliwili na kisha kutembezwa maeneo mengi.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kwa kila mpenda haki na ukombozi duniani kwa mnasaba wa kukumbuka msiba huu mkubwa wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Uislamu kwa ujumla.