EU kuunda 'chombo maalumu' cha kufanikisha biashara na Iran
(last modified Tue, 25 Sep 2018 08:06:44 GMT )
Sep 25, 2018 08:06 UTC
  • EU kuunda 'chombo maalumu' cha kufanikisha biashara na Iran

Nchi zilizosalia kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama JCPOA zimeazimia kuunda 'chombo maalumu' kitakachofanikisha mabadilishano ya kibiashara na Tehran kama sehemu moja ya kuyanusuru mapatano hayo yaliyotiwa saini Julai 2015 mjini Vienna Austria.

Hayo yamesemwa na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif walipofanya kikao na waandishi wa habari mjini New York jana Jumatatu. 

Mogherini na Zarif wameyasema hayo baada ya mkutano kati ya Iran na nchi zilizosalia kwenye makubaliano ya JCPOA, yaani Ufaransa, Ujerumani, China, Uingereza na Russia, uliofanyika mjini New York pambizoni mwa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Wanadiplomasia wa Iran na EU mjini New York

Taarifa ya pamoja ya Iran na kundi la nchi hizo liitwalo E3+2 imesisitiza kuwa, nchi zilizozalia JCPOA zitaendelea kuyaheshimu na kuyatekeleza mapatano hayo na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza wajibu wake wa kufungamana na makubaliano hayo kikamilifu, kwa ushahidi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. 

Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2018 alikariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na akatangaza kujiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hatua hiyo ilikoselewa na kupingwa vikali kote duniani hususan na nchi wanachama wa kundi la 5+1. 

Tags