EU yasisitizia udharura wa Saudia kuwekewa vikwazo vya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48596-eu_yasisitizia_udharura_wa_saudia_kuwekewa_vikwazo_vya_silaha
Wabunge wa Umoja wa Ulaya wamepiga kura kwa kishindo kuunga mkono azimio linalotaka kuwekewa vikwazo vya silaha Saudi Arabia, inayoongoza katika mauaji na hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2018 12:00 UTC
  • EU yasisitizia udharura wa Saudia kuwekewa vikwazo vya silaha

Wabunge wa Umoja wa Ulaya wamepiga kura kwa kishindo kuunga mkono azimio linalotaka kuwekewa vikwazo vya silaha Saudi Arabia, inayoongoza katika mauaji na hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen.

Wabunge wa EU jana Alkhamisi walipiga kura ya ndio kuunga mkono azimio hilo, huku wakiyataja mashambulizi ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen kuwa ni jinai za kivita.

Mmoja wa wabunge wa Bunge la EU, Angela Vallina amesema azimio hilo linazilenga nchi kadhaa za Ulaya ambazo zingali zinauuzia utawala wa Riyadh silaha, kama vile Uingereza, Ufaransa, Sweden na Uhispania.

Wabunge hao wa Umoja wa Ulaya wamezijia juu nchi wanachama wa EU kwa kuruhusu kuendelea kuuziwa silaha Saudia, hatua wanayosema inakiuka sheria ya kudhibiti mauzo ya silaha ya umoja huo.

Rais Donald Trump wa US na Mrithi wa Ufalme Saudia, Mohammad Bin Salman

Marekani inatajwa kuwa muuzaji mkubwa wa silaha kwa Riyadh, ambapo imeiuzia silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.4 tokea mwaka 2014, ikifuatiwa na Uingereza, zaidi ya dola bilioni 2.6 huku Ufaransa ikishika nafasi ya tatu kwa kurundika silaha zenye thamani ya dola milioni 475 nchini Saudia.

Saudia, kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kikatili ya pande zote dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Machi 2015, ambapo hadi sasa watu zaidi ya 12 elfu wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa mbali na mamilioni waliolazimika kuwa wakimbizi.