Uturuki: Tuna mkanda unaothibitisha Saudia imemuua Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48751-uturuki_tuna_mkanda_unaothibitisha_saudia_imemuua_khashoggi
Afisa mmoja wa masuala ya usalama wa Uturuki amesema kuwa, kuna mkanda wa sauti na video unaothibitisha kuwa mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ameuawa ndani ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Uturuki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2018 13:42 UTC
  • Uturuki: Tuna mkanda unaothibitisha Saudia imemuua Khashoggi

Afisa mmoja wa masuala ya usalama wa Uturuki amesema kuwa, kuna mkanda wa sauti na video unaothibitisha kuwa mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ameuawa ndani ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Uturuki.

Gazeti la Washington Post la Marekani limewanukuu maafisa wa nchi hiyo na wa Uturuki wakisema kuwa, mkanda huo wa video una ushahidi wa wazi kwamba maafisa usalama wa Saudi Arabia walimkamata Khashoggi baada tu ya kuingia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul, wakamtesa, kumuua na kisha wakamkatakata vipande.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, mkanda wa sauti pia unatoa ushahidi wa wazi zaidi juu ya jinsi timu ya maafisa usalama wa Saudi Arabia ilivyohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi.

Mwandishi huyo ambaye amekuwa mashuhuri kutokana na kukosoa siasa za utawala wa kifalme wa Saudia amekua akiishi nje ya nchi tangu mwaka jana akihofia usalama wake.

Jamal Khashoggi

Mkanda huo wa sauti unaeleza jinsi maafisa hao wa Saudia walivyokuwa wakimhoji Jamal Khashoggi, kumtesa na kisha kumuua.

Inaaminika kuwa baada ya kuuawa na kukatwa vipande vipande mwili wa mkosoaji huyo wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia uligawanywa katika sehemu mbili na kusafirishwa kwa ndege mbili hadi Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi alitekwa nyara tarehe 2 Oktoba akiwa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul huko Uturuki.

Jina la Jamal Khashoggi lilikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa kwa udi na uvumba na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na kwa msingi huo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema kuwa ametekwa nyara kwa amri ya Bin Salman.