Dunia yatoa radiamali baada ya Saudia kukiri kumuua Jamal Khashoggi
Saa chache baada ya Saudi Arabia kukiri kuwa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa Aal-Saud ameuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul nchini Uturuki, taasisi na viongozi mbalimbali wa kimataifa wametoa taarifa za kulaani mauaji hayo ya kikatili.
Baada ya wiki kadhaa kupita huku Saudia ikikanusha madai ya kuhusika na mauaji hayo, mapema leo imetoa taarifa na kusema kuwa Khashoggi aliuawa katika ubalozi huo wa Istanbul, eti baada ya kupigana na maafisa wa ubalozi huo, na kwamba Wasaudi 18 wanazuiliwa kufuatia mauaji hayo, huku maafisa wawili wa ngazi za juu wa ubalozi huo wakipigwa kalamu nyekundu.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake ameeleza juu ya kukerwa na kusikitishwa kwake na taarifa hiyo ya Saudia na kusema kuwa, kuna haja ya kufanyika uchunguzi huru, sambamba na kuwawajibisha wahusika wa ukatili huo.
Wanasiasa wa Marekani wakiwemo seneta wa chama cha Republican, Lindsey Graham na mwenzake wa Democrats, Adam Schiff wamesema ni jambo la kushangaza namna Saudia siku zote hizo imekuwa ikisisitiza kuwa haijahusika na mauaji hayo huku wakikisisitiza kuwa, kuna udharuru wa kubebeshwa dhima watawala wa Riyadh.
Rawya Rageh, afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International sanjari na kulaani mauaji hayo, amesema kamati iliyoundwa na Riyadh ya kuchunguza tukio hilo itaegemea upande mmoja na kwa msingi huo kuna haja ya kuundwa jopo huru la kimataifa la kuchunguza ukatili huo.
Kwa upande wake, Karen Attiah, mhariri mkuu wa makala zinazochapishwa katika gazeti la The Washington Post ameitaja taarifa ya Saudia kama tusi kwa fikra za walio wengi duniani, na kwamba haijatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu mauaji hayo wala haijatoa majibu ya masuali magumu, kama vile ulipo mwili wa Khashoggi na kwa nini maafisa wa ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul walitoa taarifa za urongo hapo awali kuhusu mauaji hayo.
Naye Kristin Diwan, afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Washington la Arab Gulf States Institute amesema ni jambo la kutiliwa shaka namna Saudia imeamua kukiri kuhusu mauaji hayo baada ya mashinikizo ya jamii ya kimataifa.