Uturuki yasema haikubaliani na 'funika-funika' mambo ya Saudia kuhusu Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48929-uturuki_yasema_haikubaliani_na_'funika_funika'_mambo_ya_saudia_kuhusu_khashoggi
Msemaji wa chama tawala cha Justice and Development Party (AK Party) cha Rais Recep Tayyid Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, Ankara haikubaliani na juhudi za kufunika funika na kuficha ukweli kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na kwamba itatumia mbinu zake zote kuhakikisha kuwa ukweli wote unafichuliwa kuhusu mauaji hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2018 12:58 UTC
  • Uturuki yasema haikubaliani na 'funika-funika' mambo ya Saudia kuhusu Khashoggi

Msemaji wa chama tawala cha Justice and Development Party (AK Party) cha Rais Recep Tayyid Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, Ankara haikubaliani na juhudi za kufunika funika na kuficha ukweli kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na kwamba itatumia mbinu zake zote kuhakikisha kuwa ukweli wote unafichuliwa kuhusu mauaji hayo.

Shirika la habari la Anadolu la serikali ya Uturuki limemnukuu msemaji wa chama cha AK Party, Omer Celik akisema hayo leo na kusisitiza kuwa, Ankara itafichua kila kitu. Hakuna mtu yeyote anayepaswa kutilia shaka suala hilo kivyovyote vile.

Amesema, sisi hatumtuhumu yeyote, lakini pia hatutaki kuona kinabakia kitu chochote kilichofichikana katika suala hilo.

Maher Abdulaziz M. Mutreb, afisa wa kijasusi wa Saudi Arabia akiingia katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul Uturuki, muda mfupi kabla ya kuuawa Jamal Khashoggi katika ubalozi huo

Baada ya wiki mbili za kukanusha mara kadhaa kwamba haikuhusika na kutoweka kwa Jamal Khashoggi, hatimaye leo Jumamosi Saudi Arabia imekiri rasmi kwamba mwandishi huyo aliuawa kwenye ubalozi wake mjini Istanbul Uturuki baada ya kutokea mapigano na maafisa usalama wa Saudia.

Tarehe pili mwezi huu wa Oktoba, Jamal Khashoggi alionekana akiingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, na hakuonekana tena akitoka. Hatimaye leo viongozi wa Saudi Arabia wametangaza rasmi kuwa aliuawa wakati akisailiwa katika ubalozi huo mdogo ingawa hata hivyo ukoo wa Aal Saud umekataa kusema ilikoupeleka mwili wa mwandishi huyo wa habari.