Uturuki: Mikono ya Bin Salman imeroa damu ya Jamal Khashoggi
Mshauri wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa mikono ya Mohammed bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ina damu ya mwandishi habari mkosoaji Jamal Khashoggi.
Ilnur Cevik amesema kuwa hiyo ni fedheha iliyompata mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia. Amesema watu wasiopungua watano walioshiriki katika timu ya mauaji ni watu wa karibu kwa Mohammed bin Salman na hawawezi kuchukua hatua bila ya yeye kujua.
Mshauri wa Rais wa Uturuki ameongeza kusema kuwa, hata kama Rais Donald Trump wa Marekani atamnusuru Mohammed bin Salman mbele ya macho ya walimwengu, lakini ndiye anayepasa kulaumiwa kuhusu mauaji ya mwandishi huyo wa habari.
Jamal Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji wa serikali ya Riyadh hususan mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman alikuwa akiandika katika gazeti la Washington Post. Mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki lakini hakuonekana akitoka.
Maafisa wa Saudia awali walisisitiza kuwa Khashoggi alitoroka katika ubalozi huo mdogo baada ya kukamilisha kufuatilia karatasi zake, hata hivyo maafisa hao hatimaye wamekiri siku 17 baada ya kutojulikana alipo mwandishi huyo wa habari kwamba aliuliwa ndani ya jengo hilo la ubalozi mdogo wa Saudia katika mabishano.
Leo Jumatano Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa nchi yake haitaruhusu wale wote waliohusika na kumuuwa Khashoggi kukwepa kukabiliwa na mkondo wa sheria akisisitiza msimamo wake wa awali kuhusu kesi hii. Amesema Uturuki imejipanga na haitaruhusu ficha ficha yoyote katika mauaji haya na wahusika wa jinai hiyo hawatakwepa mkondo wa sheria."