CNN: Kuiwekea vikwazo Iran kutaidhoofisha Marekani
Kanali ya televisheni ya Marekani CNN imeripoti kuwa, kutounga mkono Ulaya hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Iran kutazidi kudhoofisha nguvu za Marekani.
Samantha Vinograd, mchambuzi wa kanali ya televisheni ya CNN ameashiria hatua ya serikali ya rais wa Marekani Donald Trump ya kuiwekea tena vikwazo Iran na kueleza kwamba, vikwazo hivyo vya nchi hiyo ni vya ubabe na utumiaji mabavu tu.
Sambamba na uchambuzi huo, kanali ya televisheni ya CNN imeonyesha taswira za maandamano ya jana ya wananchi wa Iran ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari.
Siku ya Ijumaa iliyopita, serikali ya Marekani ilitangaza kuwa kuanzia leo Jumatatu itaanza kuiwekea tena Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vinavyohusiana na masuala ya nyuklia.
Wakati huohuo mawaziri wa mambo ya nje na wa fedha wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa pamoja na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya wametoa taarifa ya pamoja na kueleza kwamba, zimepigwa hatua kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa utaratibu wa mabadilishano ya kifedha uliopendekezwa na EU, ambao unajulikana kama SPV. Lengo la kutumiwa utaratibu huo ni kuendelezwa uhusiano wa kibiashara na kibenki kati ya Umoja wa Ulaya na Iran katika kipindi cha vikwazo vya Marekani.../