Malengo halisi ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia
(last modified Sun, 18 Nov 2018 07:02:10 GMT )
Nov 18, 2018 07:02 UTC
  • Malengo halisi ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia

Uhusiano wa Marekani na Russia tangu baada ya kumalizika Vita Baridi umekuwa na pandashuka nyingi na mivutano ya mara kwa mara. Tangu mwaka 2011 Marekani imekuwa ikiiwekea vikwazo Russia kwa kutumia visingizio mbalimbali.

Mkondo huo wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia ulishika kasi zaidi baada ya mgogoro wa Ukraine mwaka 2014 na katika kipindi cha miaka 4 iliyopita uhusiano wa nchi hizo mbili uimekuwa na mivutano mingi. Vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia vinahusu masuala mengi yakiwemo ya kisaisa, kidiplomasia, kibiashara, kijeshi, silaha na masuala ya nishati. Vifurushi vya vikwazo hivyo vya Marekani sasa vimefikia 62, na zaidi Washington inatumia mgogoro wa Ukraine kuiwekea vikwazo Russia. Vilevile mwezi Agosti mwaka jana Marekani ilianza kutekeleza vikwazo vya CAATSA dhidi ya Russia kwa kisingizio kwamba, Moscow iliingilia zoezi la uchaguzi uliopita wa Rais nchini Marekani. Vikwazo vingine vya Marekani dhidi ya Russia ni vile vinavyohusiana na madai ya kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia nchini Uingereza, Sergei Skripal na kadhia ya eneo la Crimea. Vikwazo hivyo vyote vya Marekani vimekabiliwa na majibu makali kutoka Russia.

Vladimir Putin na Donald Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov anasema, lengo la vikwazo hivyo vya Marekani ni kutaka kuyafukuza makampuni ya Russia katika masoko ya kimataifa na hatimaye kukwamisha ustawi wa kiuchumi wa nchi hiyo. Maafisa wa serikali ya Moscow pia wamekuwa wakisisitiza kuwa vikwazo hivyo hususan vile vinavyolenga sekta ya nishati ni kutaka kuizuia Russia isiwepo katika masoko ya gesi ya Ulaya ambayo asilimia yake zaidi ya 30 inadhibitiwa na makampuni ya Russia. Mwenendo huo umekabiliwa na upinzani hata kutoka kwa washirika wa Ulaya wa serikali ya Washington ikiwemo Ujerumani. Kwa sasa Wajerumani wako chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani inayotaka kusitishwa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi wa Nord Stream II ambalo litasafirisha gesi ya Russia kuelekea Ujerumani kupitia Bahari ya Baltic. Kuhusu suala hilo Lavrov anasema: Mbinu mbalimbali za mashinikizo ya kiuchumi kama kutoa tahadhari na vitisho vya White House hazihusu Russia pekee bali zinatumika hata dhidi ya waitifaki wa Marekani.

Marekani inataka kuilazimisha Russia isalimu amri mbele ya matakwa yake na jambo hilo limesisitizwa mara kwa mara na Rais wa nchi hiyo, Donald Trump. Viongozi wa Russia wanasema kuwa, vikwazo hivyo vya Marekani vina taathira mbaya si kwa Moscow pekee bali kwa dunia nzima. Rais Vladimir Putin wa Russia anasema kuweka vikwazo na vizuizi vya biashara ya kimataifa kuna madhara kwa pande zote na kuongeza kuwa: Hata wawekaji wa vikwazo hivyo wenyewe ikiwemo Marekani wanasumbuliwa na athari zake mbaya.

Russia imechukua hatua kadhaa ili kupunguza utegemezi wake kwa sarafu ya dola ya Marekani na kwa njia hiyo iweze kuopungzua madhara ya vikwazo vya serikali ya Washington kwa uchumi wa nchi hiyo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha mfumowa SWIFT wa Kirusi na kupanua zaidi biashara na nchi ya China.

Gavana wa Benki Kuu ya Russia, Elvira Nabiullina anasema kuwa: Moscow imeandaa mazingira yote yanayohitajika kwa ajili ya kudumisha harakati za kibenki za Russia iwapo nchi hiyo itaondolewa katika mfumo wa sasa wa SWIFT unaodhibitiwa na Marekani.

Sambamba na hayo Russia inafanya jitihada za kushirikisha nchi nyingine kama India, Iran na Uturuki katika mahusiano na miamala yake ya kifedha na kibiashara isiyotegemea sarafu ya dola ya Marekani.