Nov 21, 2018 07:53 UTC
  • Shambulizi la kigaidi laua watu 50 wakisherehekea Maulidi Afghanistan

Watu wasiopungua 50 wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga mkusanyiko wa Waislamu waliokuwa katika sherehe za Maulidi ya Mtume Muhammad (SAW) katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Kanali ya televisheni ya Tolo imeripoti kuwa, shambulizi hilo lilitokea ndani ya Ukumbi wa Uranus mjini Kabul, uliokuwa umekusanya watu zaidi ya elfu moja wakiadhimisha kumbukumbu ya mazazi ya Mtukufu Mtume jana jioni, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50.

Duru za habari zinaarifu kuwa, gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu aliingia ukumbuni hapo na kujiripua, na kusababisha maafa hayo, huku makumi ya watu wengine wakijeruhiwa.

Hospitali ya Dharura ya Kabul imesema watu 40 wamejeruhiwa vibaya kwenye hujuma hiyo ya kigaidi iliyolenge waumini wa Kiislamu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya sherehe za Maulid zilizoanza jana Jumanne katika kona mbalimbali za dunia.

Manusura wa shambulizi la Kabul wakibebwa na ambulensi

Rais Ashraf Ghani ametangaza leo Jumatano kuwa siku ya kitaifa ya kuwaomboleza wahanga wa jinai hiyo ya kigaidi. Ingawaje hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo kufikia sasa, lakini mashambulizi ya kikatili ya aina hii yamekuwa yakifanywa na wanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Katikati ya mwezi uliopita wa Oktoba, makumi ya watu wenginre waliuawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kampeni za uchaguzi, kaskazini mashariki mwa Afghanistan. 

 

Tags