Jitihada za kuboresha hali za wahajiri duniani
Mkutano wa kimataifa wa uhajiri ulianza jana Jumatatu ya tarehe 10 Desemba nchini Morocco katika hali ambayo, mazingira na hali isiyoridhisha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, pamoja na kukosekana usalama katika nchi mbalimbali duniani hususan za mabara ya Afrika na Amerika ya Latini na maeneo mengine kadhaa ya bara la Asia vimesababisha kuongezeka wimbi la wahajiri duniani.
Kwa mujibu wa takwimu, akthari ya wahajiri hao ni vijana na wanawake, ambao wamezihama nchi zao kwa ajili ya kutafuta maisha bora katika nchi zingine. Kuhusiana na jambo hilo, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umetangaza kuwa, zaidi ya nusu ya vijana na vijana chipukizi wenye umri wa miaka 14 hadi 24 wamezihama nchi zao kutokana na ufakiri na hali mbaya mno ya maisha.
Wimbi la wahajiri limeongezeka zaidi duniani katika miaka ya karibuni. Ongezeko la migogoro ya kisiasa, kukosekana demokrasia, kuwepo watawala madikteta hususan katika baadhi ya nchi za Afrika, hali mbaya ya uchumi, kutokuwepo nafasi za ajira, kuongezeka ughali wa maisha, kukosekana usalama wa chakula na kushamiri harakati za makundi ya kigaidi yanayovuruga usalama, zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya raia wa nchi nyingi hasa za Afrika, Amerika ya Latini na magharibi ya Asia wazihame nchi zao.
Kwa upande mwingine, siasa na sera za nchi za Magharibi na uingiliaji wao katika masuala ya nyingi kati ya nchi hizo, kuzibana nchi hizo ili zibaki nyuma kimaendeleo, uungaji mkono wao kwa makundi ya kigaidi na watawala vibaraka na madikteta, sambamba na kuongezeka kiwango cha mwamko na uelewa wa watu kwa kubadilika mazingira, vimesababisha kuibuka wimbi la uhajiri kuelekea nchi za Ulaya na Marekani.
Joseph Nevins, mtaalamu wa masuala ya Amerika ya Kati anaizungumzia hali hiyo kwa kusema: Uhajiri wa watu wanaotoka nchi za Amerika ya Latini kuelekea Marekani, zaidi umetokana na ushawishi mkubwa mno na uingiliaji uliofanywa na Washington kwa miongo kadhaa katika nchi hizo.
Hii ni katika hali ambayo, kinyume na zinavyojaribu kuonyesha kuwa zinajali na kutetea misingi ya utu na ubinadamu, serikali za Magharibi zinawazuia wahajiri kuingia katika nchi zao. Na ndiyo maana nchi nyingi za Ulaya zimeamua kufunga mipaka yao na kuweka sheria kali na ngumu za uhajiri. Katika mpaka wa pamoja wa Mexico na Marekani pia ambako kunashuhudiwa umati mkubwa wa wahajiri kutoka nchi za Amerika ya Latini, kuna vikosi vya askari waliojizatiti kukabiliana na wahajiri hao.
Judith Sunderland, mkurugenzi wa kitengo cha Ulaya na Asia ya Kati cha shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch analizungumzia suala hilo kwa kusema: Sera za sasa za Umoja wa Ulaya kuhusu wahajiri na hatua zisizo za uhakika za kuwapatia makazi na maskani wakimbizi hao vimewazidishia machungu na mateso watu hao, kiasi kwamba nchi wanachama wa Umoja wa UIaya zimefika hadi ya kukwamisha shughuli za kuwaokoa wakimbizi waliokwama baharini, zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali, meli za biashara na hata meli za kijeshi.
Hivi sasa hali ya wahajiri si ya kuridhisha. Akthari yao wanakwama mipakani wakibaki wanangoja kwa miezi kadhaa, huku wengine wengi wakinaswa na magenge ya wafanya magendo ya binadamu, mbali na wale wanaopoteza maisha kwa kughariki kwenye maji ya bahari ya Mediterania.
Katika mkutano wa kimataifa wa uhajiri unaofanyika nchini Morocco, nchi nyingi washiriki zinatazmaiwa kusaini hati rasmi ya mkataba wa kimataifa wa uhajiri. Mkataba huo wa kimataifa ulioandaliwa na kuratibiwa kwa umakini kwa ajili ya kuunga mkono uhajiri salama, unatilia mkazo misingi na haki zilezile zilizopo kuhusiana na uhajiri; yaani kutetea haki za kiutu hususan za wanawake na watoto wadogo. Japokuwa mkataba huo hauna dhamana na hakikisho la utekelezaji, lakini baadhi ya nchi ikiwemo Marekani, tayari zimetangaza kuwa hazitaukubali.
Mazingira kwa ajili ya wahajiri na nchi wanakoelekea ni mabaya mno; na inavyoonekana, uwekaji sera kali unaofanywa na nchi hizo haujawa suluhisho, bali kuna haja ya kuchukuliwa hatua mpya, ikiwemo ya kutazamwa upya sera za uchumi na maendeleo za Magharibi kuhusiana na nchi zingine.
Kuhusiana na suala hilo, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya anasema: Njia pekee ya kuibadilisha dunia yetu kuelekea dunia iliyo bora, ni kushirikiana kwa ajili ya kuufikia mfumo wa dunia wa ushirikishaji.../