WikiLeaks: Balozi za Marekani duniani zimerundika vifaa vya ujasusi
(last modified Sun, 23 Dec 2018 08:11:59 GMT )
Dec 23, 2018 08:11 UTC
  • WikiLeaks: Balozi za Marekani duniani zimerundika vifaa vya ujasusi

Mtandao wa WikiLeaks umefichua kuwa, balozi za Marekani na vituo vingine vyake vya kidiplomasia kote duniani vimenunua kiwango kikubwa cha vifaa na suhula za kijasusi; katika hali ambayo baadhi ya nchi zimekuwa zikieleza hofu yao kwamba balozi hizo za Marekani badala ya kujihusisha na masuala ya udiplomasia pamoja na uhusiano mwema, zinahusika zaidi na masuala ya ujasusi, mapinduzi ya serikali halali na njama zinginezo haribifu kote duniani.

Wikileaks imefichua kuwa, kuna maombi zaidi ya 16,000 kutoka balozi na balozi ndogo za Marekani za kutaka kununuliwa bidhaa hizo za kijasusi katika pembe mbalimbali ya dunia. 

Kwa mujibu wa mtandao wa WikiLeaks ambao ni maarufu kwa kufichua uozo na ufisadi wa serikali mbalimbali duniani, orodha ya bidhaa zilizonunuliwa na zinazotaka kununuliwa na balozi za Marekani ni kalamu, kofia, tai, saa na vifungo vya shati vyenye kamera za kijasusi. 

Mtandao huo umetoa mfano wa hivi karibuni, ambapo balozi za Marekani katika nchi za Panama, el-Salvador na Colombia zilinunua mamia ya vifaa hivyo vya kijasusi, kana kwamba ni vitu vya matumizi ya kawaida ya kiofisi.

Mtandao wa kufichua ufisadi wa Wikileaks

Hivi karibuni, Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema historia ya sasa imejaa mifano ya harakati zilizo kinyume cha sheria na kinyume cha kanuni za kimataifa ambazo hufanyika katika balozi za Marekani duniani na hivyo kuvuruga uhusiano na nchi wenyeji kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.

Alisema ushahidi unaonyesha kazi haribifu ambazo hufanywa na mamia ya maafisa wa kijeshi na kijasusi wa Marekani ambao hufanya shari zao kwa jina la wanadiplomasia.