Russia: Marekani inakiuka azimio la UN kuhusu Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50400-russia_marekani_inakiuka_azimio_la_un_kuhusu_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa Marekkani inaendelea kukiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kujitawala na uhuru wa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2018 23:27 UTC
  • Russia: Marekani inakiuka azimio la UN kuhusu Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa Marekkani inaendelea kukiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kujitawala na uhuru wa Syria.

Sergey Lavrov amesema kuwa licha ya madai kwamba wanataka kuondoa majeshi yao katika ardhi ya Syria, Wamarekani wamekuwa wakikiuka mara kwa mara mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, askari wa Marekani walioko Syria hawapigani vita, lakini wanawaudhi wengine na hata wao wenyewe; hivyo Washington inafanya jitihada ili kuondoka kwa majeshi yake nchini Syria kusitambuliwe kuwa ni "kukimbia medani ya vita". 

Lavrov pia ametahadharisha kuhusu sera za kujichukulia maamuzi na hatua za upande mmoja za Marekani ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika makubaliano ya silaha za nyuklia ya INF na kusema kuwa: Sera hizo zitazidisha mashindano ya silaha na kutayarisha mazingira ambayo matokeo yake yatakuwa makosa makubwa na yenye maangamizi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, Marekani na washirika wake wanadumisha sera zao za kibabe na hawako tayari kukubaliana na hali halisi ya dunia ya sasa ambayo ni kinyume na maslahi yao.