China yapasisha "kukomunistishwa" utamaduni wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50716-china_yapasisha_kukomunistishwa_utamaduni_wa_kiislamu
Serikali ya China imepasisha sheria ya kuoanisha utamaduni wa Kiislamu na mafundisho ya kikomunisti.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 07, 2019 23:07 UTC
  • China yapasisha

Serikali ya China imepasisha sheria ya kuoanisha utamaduni wa Kiislamu na mafundisho ya kikomunisti.

Maafisa wa serikali ya China ambao wamekutana na wawakilishi wa jumuiya nane za Waislamu wa nchi hiyo, wamekubaliana kwamba, Uislamu unapaswa kuoanishwa na ukomunisti na kuchukuliwe hatua za kufananishwa Uislamu na mila na utamaduni wa Kichina. Ripoti zinasema kuwa, hakujatolewa habari zaidi juu ya jinsi hatua hizo zilizochukuliwa katika fremu ya kuwakandamiza Waislamu wa jamii ya Uyghur nchini humo zitakavyotekelezwa.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, Waislamu karibu milioni moja wa jamii ya Uyghur wanashilikiwa katika kambi za mafundisho ya ukomunisti katika jimbo la Xinjiang. Gay McDougal ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kupambana na Ubaguzi ya Umoja wa Mataifa ameripoti kuwa: Waislamu milioni moja wa Uyghur katika jimbo la Xinjiang nchini Uchina wanashikiliwa katika kambi zilizoko maeneo ya mbali ambako wanatwishwa mitazamo makhsusi ya kisiasa na kulazimishwa kuacha dini yao.

Ni vigumu sana nchini Uchina kutekeleza sheria na ibada za Kiislamu na wanaotekeleza sheria hizo wanaandamwa na kusumbuliwa. Pamoja na hayo inaonekana kuwa serikali ya China imefikia natija kwamba, kuweka sheria kali dhidi ya ada na desturi za Kiislamu pekee hakuwezi kupunguza changamoto zinazoikabili serikali ya Beijing katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu nchini humo na kwamba kuna uwezekano pia kwamba huenda kukapelekea kujitokeza makundi yenye misimamo mikali nchini humo. Kwa sababu hiyo na kwa kushirikiana na baadhi ya jumuiya za Waislamu, China inataka kujionesha kwamba, ina misimamo laini kuhusiana na masuala yanayohusiana na Waislamu.

Nicholas Marogan ambaye ni mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anasema kuhusu mienendio ya serikali ya China dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uyghur kwamba: China inapaswa kusitisha mwenendo wa kuwatia nguvuni watu wa jamii za waliowachache na kuacha kuwashikilia katika kambi za kulazimishwa kwa sababu suala hilo halina mashiko ya kisheria.

Vilevile hatua ya serikali ya China ya kutaka kuoanisha Uislamu na Ukomunisti ni suala muhali na lisilowezekana. Hii ni kwa sababu, Uislamu ni dini yenye kitabu na sheria za Mwenyezi Mungu zisizoweza kubadilishwa na wala hauwezi kuoanishwa au kulinganishwa na mafundisho ya kisiasa ya mfumo wa aina yoyote ile wa wanadamu. Kwa msingi huo badala ya serikali ya China kutaka kubadilisha Uislamu na kuuoanisha na mafundisho ya Kikomunisti inapasa kutumia mafundisho na sheria za dini hiyo katika kurekebisha masuala ya watu wa nchi hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Uislamu ndiyo dini kamili zaidi ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wanadamu wote na ina sheria na kanuni zote zinazohitajiwa na wanadamu.

Mhadhiri wa historia wa Chuo Kikuu cha Georgetown nchini Marekani, James Millwright anasema: "Huko Uchina wanazitambua itikadi za kidini kuwa ni jambo lisilofaa. Beijing inadai kuwa, dini inastawisha na kueneza misimamo mikali na itikadi za kutaka kujitenga, kwa sababu hiyo kambi za kutoa mafunzo mapya ya kikomunisti nchini humo zimepewa jina la "hospitali" za kutibu fikra na itikadi."

Waislamu wanabinywa na kukandamizwa Xinjiang, Uchina

Ukweli ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China imepatwa na wasiwasi mkubwa wa kuingia fikra za makundi yenye misimamo mikali katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu likiwemo jimbo la Xinjiang. China imeona kuwa, siasa za kutumia mabavu, kuwatia nguvuni na kuwabinya Waislamu na hata kuvuruga muundo wa kijamii wa raia hao havikuweza kupunguza wasiwasi wake. Hivyo imeamua kushirikiana na jumuiya za Waislamu nchini humo. Serikali ya Beijing inaelewa vyema kwamba, kuna baadhi ya wanachama wa makundi yenye misimamo mikali wanaoungwa mkono na kusaidiwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao wanasafirishwa kupitia Afghanistan kuelekea maeneo ya Asia ya Kati na Kaukazia. Kwa msingi huo kukabiliana kwa mkono wa chuma na Waislamu wa China ambao takwa lao kuu ni kuwa na uhuru wa kutekeleza ibada zao za kidini hakuwezi kupunguza wasiwasi wa Beijing katika suala la kupambana na makundi yenye misimamo mikali.

Kwa kuzingatia hayo yote duru za kisiasa nchini Uchina zinasema serikali ya nchi hiyo inalazimika kupanua zaidi ushirikiano wake na Waislamu wa nchi hiyo na kutumia uzoefu wao kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na kuungwa mkono na Marekani.