Russia yaionya Marekani na kuitaka iondoe manowari zake Bahari Nyeusi
Russia imeionya vikali Marekani na kuotaka iondoe meli yake ya kivita ya USS Donald Cook ambayo iko katika Bahari Nyeusi.
Russia imesema inafuatilia kwa karibu harakati za meli hiyo ya kivita na imeitahadahrisha kuwa isikaribie pwani yake.
Senata wa ngazi za juu nchini Russia, Alexei Pushkov amesema meli za kivita za Marekani zinazotembelea Bahari Nyeusi hazifanyi hivyo kwa ajili ya usalama wa Marekani bali kwa ajili ya sera za ndani za Marekani. Marekani imedai meli yake hiyo ya kivita inatekeleza oparesheni za baharini kwa lengo la kuimarisha usalama.
Hali katika eneo hilo ni tete kutokana na mzozo baina ya Russia na Ukraine ambapo Marekani inaunga mkono Ukraine katika mzozo huo.

Serikali ya Russia imezitaka nchi nchi za Magharibi hasa Marekani kuacha kuchochea mzozo kati yake na Ukraine. Uhusiano kati wa Russia na Ukraine uliharibika mwaka 2014 baada ya wanasiasa wanaofuata madola ya Magharibi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya muda ya Ukraine. Aidha hatua ya kisiwa cha Crimea kuitisha kura ya maoni ya kujitenga na Ukraine na kujiunga na Russia mwaka huo huo, ilizidisha mgogoro baina ya nchi hizo.