Mkuu wa Rossiya Segodnya ataka kuachiwa huru Marzieh Hashemi
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la habari la kimataifa la Rossiya Segodnya la Russia amesema kuwa kuna udharura wa vyombo vyote huru vya habari duniani kumtetea na kumuunga mkono mwandishi habari wa televisheni ya Press TV, Marzieh Hashemi anayeshikiliwa na vyombo vya usalama vya Marekani.
Dmitry Kiselyov amezungumzia hatua ya Marekani ya kumtia nguvuni Marzieh Hashemi na kusisitiza kuwa, Marekani daima imekuwa ikitumia sera ya utekaji nyara wa kisiasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Rossiya Segodnya amesema kuwa maafisa wa serikali ya Marekani huwa wanalipiza kisasi kwa raia wa kawaida na mara hii wamemlenga mwandishi habari na mtangazaji wa televisheni ya Iran ya Press TV.
Bi Marzieh Hashemi, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, aliyekuwa akiitwa Melanie Franklin na baadaye akakubali dini tukufu ya Uislamu, alitiwa nguvuni Jumapili ya tarehe 13 Januari katika Uwanja wa Ndege wa St. Louis, Missouri na kupelekwa mjini Washington DC ambako amewekwa kizuizini. Siku ya Ijumaa, Mahakama ya Marekani ilitangza kuwa Marizieh Hashemi alikamatwa ili atoe ushahidi mahakamani.
Siku chache silizopita mahakama moja ya Washington nchini Marekani imethibitisha kuwa mtangazaji huyo wa televisheni ya Press TV, amewekwa kizuizini bila ya kosa lolote na kwa anwani ya "shahidi muhimu" katika kesi ambayo haikutajwa.
Bi Marzieh Hashemi alikuwa safarini Marekani kumtembelea kaka yake ambaye ni mgonjwa pamoja na jamaa wengine wa familia yake.