WMO: Joto linaongezeka duniani, maafa yanazidi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa duniani, WMO limesema ongezeko la viwango vya joto ni ishara ya wazi ya mabadiliko ya tabianchi ya muda mrefu, huku likisema miaka minne iliyopita viwango vilikuwa vya kipekee.
WMO katika taarifa imesema miaka ya 2015, 2016, 2017 na 2018 imekuwa ya joto jingi ikisema kuwa ni “ishara ya wazi kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea.”
Uchambuzi wa WMO unaonyesha kuwa viwango vya wastani vya nyuzi joto kwa vipimo vya selsiasi kilikuwa ni 1,0 juu ya viwango vya kabla ya miaka ya kuanzishwa kwa viwanda 1850 hadi 1900.
Akizungumzia mwenendo wa hali ya hewa, Katibu Mkuu wa WMO, Petteri Taalas amesema mwenendo wa muda mrefu ni muhimu kuliko uchunguzi wa mwaka mmoja mmoja na kwamba taswira inaonyesha kuwa viwango vya joto vinapanda akisema, “miaka 20 iliyokuwa na joto jingi zaidi imekuwa miaka 22 iliyopita. Viwango vya joto katika kipindi cha miaka minne iliyopita vimekuwa vya aina yake nje na ndani ya bahari".
Taalas amesema viwango vya joto ni kiungo tu kwenye taswira nzima kwani athari kubwa na mbaya zinazotokana na hali ya hewa viliathiri nchi nyingi na mamilioni ya watu na kusababisha athari mbaya kwenye uchumi na mazingira mwaka 2018. Kati ya athari mbaya za ongezeko la joto duniani ni njaa, ukame, mafuriko na kuongezeka kina cha bahari na hivyo kuangamiza idadi kubwa ya visiwa na maeneo ya pwani.

Kwa mujibu wa WMO, matukio mengi ya hali ya hewa yanaambatana na matokeo ya moja kwa moja ya mabadilko ya tabianchi na hivyo ni muhimu kukabiliana na visababishi.
Hii ni katika hali ambayo, mwezi Juni mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015, akisema kuwa makubaliano hayo hayana faida yoyote kwa Marekani. Hii ni licha ya wataalamu wa mambo kuonya kwamba, hatua hiyo ya Marekani inaweza kusababisha ongezeko kubwa la joto na uharibifu wa hali ya hewa duniani.
Makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yalifikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 na kutiwa saini na nchi 194 kwa lengo la kuzuia uchafuzi wa mazingira ambao sasa umegeuka na kuwa janga linalohatarisha mustakabali wa sayari ya dunia.