Marekani yaendelea kurundika silaha Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51668-marekani_yaendelea_kurundika_silaha_mashariki_ya_kati
Afisa mwandamizi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) amesema asilimia 50 ya silaha zilizouzwa na Marekani mwaka jana 2018, zilinunuliwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 20, 2019 02:40 UTC
  • Marekani yaendelea kurundika silaha Mashariki ya Kati

Afisa mwandamizi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) amesema asilimia 50 ya silaha zilizouzwa na Marekani mwaka jana 2018, zilinunuliwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Luteni Jenerali Charles Hooper, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama ya Marekani (DSCA) amesema nchi za Mashariki ya Kati mwaka jana pekee zilinunua silaha na zana za kijeshi za Marekani zilizokuwa na thamani ya dola bilioni 30, kati ya dola bilioni 55 ilizouza nje ya nchi.

Hooper ameyasema hayo katika Kongamano na Maonyesho ya Kimataifa ya Ulinzi mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu na kuongeza kuwa, Marekani iko mbioni kuhakikisha kuwa inaongeza maradufu kiwango hicho cha mauzo ya silaha zake kwa nchi za Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa ripoti na chunguzi mbalimbali, hakuna nchi inayoipiku Saudia katika ununuzi wa silaha za Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Utawala wa Aal-Saud mwaka 2017 ulitumia zaidi ya dola bilioni 69.4 kujiimarisha kijeshi

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), Saudia ni kati ya nchi tatu zilizoongoza duniani kwa ununuzi wa silaha mwaka 2017, na pia ilishika nafasi ya tatu iliyokuwa ikishikiliwa na Russia, katika kuelekeza mapato yake mengi kwenye matumizi ya kijeshi na hususan ununuzi wa silaha.

Itakumbukwa kwamba, akiwa ziarani mjini Riyadh mwaka 2017, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Saudi Arabia itanunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 110 kutoka Marekani.