Kukiri Umoja wa Mataifa kwamba Israel inayasaidia magenge ya kigaidi
Ofisi ya António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imekiri kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel unayasaidia magenge ya kigaidi.
Uhakika usio na shaka ni kwamba, Israel ndiye muasisi wa ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa upande mmoja kitendo tu cha kuundwa dola pandikizi la Israel katika ardhi walizoporwa Wapalestina chenyewe ni ugaidi. Na kwa upande wa pili kuendelea kuwepo hadi hivi sasa dola hilo vamizi kwa uungaji mkono wa madola ya kibeberu kuna mfungamano wa moja kwa moja na ugaidi. Miongoni mwa jinai kubwa za kigaidi zilizofanywa na Wazayuni ni pamoja na mauaji ya umati ya Dir Yasin, Sabra na Shatila na Mauaji ya Ghaza ambapo kila moja ya jinai hizo ni miongoni mwa jinai kubwa zaidi kuwahi kutokea ulimwenguni.
Zaidi ya hayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiwateka nyara watu maarufu pamoja na kuendesha mauaji ya kigaidi yaliyopangiliwa vizuri dhidi ya viongozi na wasomi waliobobea katika elimu na fani mbalimbali wakiwemo wanasayansi wa Iran na viongozi wa harakati za muqawama huko Lebanon na Palestina na huo ni ushahidi mwingine wa ugaidi wa kuchupa mipaka wa Israel. Kwa kweli magenge ya kigaidi ambayo leo hii yanaendesha mashambulizi na vitendo vya kigaidi katika sehemu mbalimbali za ndani na nje ya eneo la Mashariki ya Kati yanaendeleza jinai zile zile za utawala wa Kizayuni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) akasema kuwa, Israel ndiye mama wa ugaidi.
Naye Mohammad Poor Ghulami, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati ameandika kuwa, Israel ni dola la magaidi, na sehemu kubwa ya viongozi wake ndio wanaotoa amri za moja kwa moja za kufanyika jinai kubwa za kigaidi.
Suala jingine ni kwamba, hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na wimbi la magenge ya kigaidi ambayo yanaungwa mkono moja kwa moja na Israel. Hadi hivi sasa kumeshatolewa ripoti nyingi za uhakika zinazoonesha jinsi magaidi wanaojeruhiwa katika nchi mbalibali kama huko Syria wanavyopewa matibabu na kutembelewa na viongozi wa Israel akiwemo Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo wa Kizayuni.
Gazeti la Jerusalem Post limeandika kuhusu msimamo huo mpya wa Umoja wa mataifa kwamba, ofisi ya António Guterres imeandaa ripoti kuhusu uungaji mkono wa Israel kwa magenge ya kigaidi. Ripoti hiyo itakayojadiliwa katika kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa inasema kuwa, Israel inayapa silaha, fedha na matibabu magenge ya kigaidi likiwemo la Tahrir al Sham lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida ili yaendelelee kutia hofu katika safu za wananchi wa Syria.
Amma suala muhimu zaidi hapa ni kwamba, msimamo ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati ni wa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Msimamo huo umepandisha kiburi cha utawala wa Kizayuni ambao ni nembo ya ugaidi wa kiserikali duniani na ni utawala ambao haufichi uungaji mkono wake kwa magenge ya kigaidi ambayo ni hatari kwa hata nchi zenyewe za Kiarabu zinazopigana vikumbo katika kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel.
Uhakika wa mambo ni kwamba, Israel ni dhihirisho la wazi kabisa la ugaidi wa kiserikali katika eneo hili. Ijapokuwa kukiri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwamba Israel inayaunga mkono magenge ya kigaidi ni hatua nzuri, lakini siasa za kusema kwa maneno tu haziwezi kuizuia Israel kuendelea na jinai zake za kuendesha na kuunga mkono vitendo vya kigaidi. Inavyoonekana ni kwamba msimamo huo wa Umoja wa Mataifa umechukuliwa kwa ajili tu ya kukabiliana na misimamo ya kuchupa mipaka ya Marekani inayoiunga mkono kibubusa Israel.