Jarida la Marekani: Trump amepelekea nchi yetu itengwe na Ulaya
Jarida moja la nchini Marekani limemlaumu vikali rais wa nchi hiyo, Donald Trump kwa siasa zake mbovu za kimataifa na kusema kuwa, Trump amepelekea Marekani itengwe na nchi za Ulaya.
Jarida hilo la Foreign Affairs limesema hayo katika ripoti yake ya jana na kuongeza kuwa, katika wakati ambapo nchi za Ulaya zilikuwa na matarajio makubwa sana ya kufaidika na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, Trump alichukua uamuzi wa kipumbavu wa kuitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kupelekea waitifaki muhimu wa Washington wajitenge na Marekani.
Ripoti ya jarida hilo imeongeza kuwa, hatua za kipumbavu zinazochukuliwa na Trump kama vile kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA zimewakatisha tamaa hata waitifaki wa karibu na wa kihistoria wa Marekani.
Limeongeza kuwa, Iran na suala la kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA ndio msingi mkuu wa mzozo baina ya Marekani na waitifaki wake wakuu yaani nchi za Ulaya.
Vyombo vya habari vya Magharibi vinauhesabu msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kulinda mapatano ya JCPOA kwamba ni kwa manufaa ya Iran na ni pigo kwa Marekani.
Donald Trump amekuwa akijitoa kwenye mapatano mbalimbali ya kieneo na kimataifa na siasa hizo mbovu zimeifanya Marekani itengwe na mataifa yote ya dunia ambayo yanaiona haina mwamana na haiheshimu hata ahadi inazozitoa kwa hiari yake yenyewe.
Mbali na kujitoa katika mapatano ya JCPOA, Trump ameitoa Marekani pia katika mikataba mingine kadhaa kama ule wa hali ya hewa wa Paris, mkataba wa Asia na Pasifiki na mkataba wa biashara huru ya Amerika Kaskazini.