Aliyekuwa msaidizi wa Papa Francis afungwa kwa kulawiti watoto
(last modified Wed, 13 Mar 2019 07:47:46 GMT )
Mar 13, 2019 07:47 UTC
  • Aliyekuwa msaidizi wa Papa Francis afungwa kwa kulawiti watoto

Mahakama moja nchini Australia imemhukumu kifungo cha miaka sita jela, aliyekuwa Mkuu wa Hazina ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani Vatican, Kadinali George Pell.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya dakika 60 hii leo, Jaji wa Mahakama ya Jimbo la Victoria nchini Australia, Peter Kidd amesema, "Kwa matazamo wangu, kiburi cha hali ya juu ndicho kilichokufanya utende jinai hiyo. Ulikuwa na muda wa kujitathmini na kujirudi, lakini hukuacha kufanya ufuska huo." 

Hukumu ya juu ya hatia aliyopatikana nayo kiongozi huyo wa zamani wa Kanisa Katoliki na mpambe wa zamani wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, ni kifungo cha hadi miaka 50 jela.

Kadinali Pell mwenye umri wa miaka 77 ndiye kiongozi wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki kuhukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi watoto wadogo wa kiume, katika shule moja ya Ballarat eneo la Torquay alipokuwa padri wa Kanisa la Kikatoliki la St Patrick's mjini Melbourne.

Kadinali Pell akitoka mahakamani

Julai mwaka jana, Philip Wilson, Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini Australia alijiuzulu kutokana na kuficha taarifa kuhusu jinai za kingono zilizofanywa na padri mmoja dhidi ya watoto ndani ya kanisa, wiki chache baada ya kujiuzulu Kadinali Theodore McCarrick, mmoja wa viongozi muhimu wa kanisa katoliki nchini Marekani ambaye anakabiliwa na kashfa ya ngono.

Viongozi wa Kanisa Katoliki mjini Vatican wamekiri kuwa ufisadi wa kimaadili umekuwa ukikithiri katika makanisa mbalimbali ya madhehebu ya Katoliki duniani.