Kuchukua wigo wa kimataifa mgogoro wa kisiasa wa Venezuela
(last modified Sun, 07 Apr 2019 07:03:46 GMT )
Apr 07, 2019 07:03 UTC
  • Kuchukua wigo wa kimataifa mgogoro wa kisiasa wa Venezuela

Mgogoro wa kisiasa wa sasa nchini Venezuela ulianza 10 Januari mwaka huu wakati Rais Nicolas Maduro alipoapishwa baada ya kushinda katika uchaguzi wa Rais uliosusiwa na wapinzani na hivyo kuchukua usukani wa kuiongoza nchi hiyo katika duru ya pili.

Mgogoro huo ulishadidi zaidi Januari 23 mwaka huu baada ya Juan Guiado, kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo ambapo Marekani na akthari ya nchi za Ulaya la Amerika ya Latini zilitangaza kumuunga mkono mpinzani huyo. Mkabala na hilo nchi kama Russia, Iran, China, Uturuki, Bolivia na Mexico zililaani vikali hatua hiyo ya Guaido na kutangaza kumuunga mkono Nicolas Maduro.

Hivi karibuni pia, Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani naye alisisitiza kuwa, nchi yake itaunda muungano wa kimataifa dhidi ya Maduro ili umlazimishe aachie madaraka. Kwa hakika matamshi haya ni mlolongo wa senario iliyoanzishwa na Marekani na waitifaki wake wa Ulaya na wa Kiarabu, ambayo ilianza kutekelezwa huko Syria mwaka 2011 lengo likiwa ni kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad. Hata hivyo, Marekani na washirika wake wamegonga mwamba na kushindwa kufikia malengo yao huko nchini Syria.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela

Suala hilo limewafanya viongozi wa ngazi za juu wa Venezuela wawe mbioni kustafidi na tajiriba na uzoefu wa Syria kwa ajili ya kukabiliana na Marekani.

Akihutubia katika Chuo Kikuu cha Damascus hivi karibuni, Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela sambamba na kubainisha kwamba, nchi yake inakabiliwa na njama zinazoshabihiana na zile za miaka minane dhidi ya Syria amesema kwamba: Caracas inatumia mbinu na mkakati wa Syria wa kusimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na ubeberu.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela ameashiria hasira za Marekani kutokana na kushindwa kufaulu njama zake dhidi ya serikali ya Caracas na kusema bayana kwamba, vikwazo na hatua za upande mmoja za Marekani za kuwazingira wananchi wa Venezuela zinaonyesha kuwa, misimamo ya marafiki wa Caracas  mbali na wananchi na serikali kama za Russia, China, Iran, Syria, Serbia na Belurus imeimarisha nguzo na misingi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Matamshi hayo ya Jorge Arreaza ni ishara ya kuchukua mkondo wa kimataifa mgogoro wa kisiasa wa Venezuela na kuibuka kambi za kimataifa ikiwemo inayoipinga serikali ya Caracas na nyingine ikiiunga mkono serikali hiyo.

Rais Nicolas Maduro

Mwanzoni mwa mgogoro huo, serikali ya Washington ilidhani kwamba,  kama ilivyokuwa huko nyuma hususan katika kipindi cha vita baridi ingeweza kuiondoa kirahisi madarakani serikali ya Nicolas Maduro kwa kutumia mabavu na kuchukua hatua za kihasama dhidi ya nchi hiyo.

Hata hivyo upinzani mkali wa mataifa mengine makubwa hususan Russia na China na hatua ya mataifa hayo ya kumuunga mkono Maduro sambamba na kutuma vikosi vya kijeshi huko Venezuela, imetuma ujumbe ulio bayana kwa viongozi wa Washington kwamba, zama za uchukuajia hatua za upande mmoja za Marekani kwa ajili ya kufikia malengo yake zimepitwa na wakati.

Hatua ya Russia na China ya kutuma majeshi yao huko Venezuela ni ujumbe wa wazi kabisa kwa serikali ya Trump kwamba, Beijing na Moscow zitakabiliana na njama za Marekani dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani

Jambo hilo limeikasirisha mno serikali ya Marekani. Akizungumza Alkhamisi iliyopita mwishoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO),Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alitangaza kuwa, suala la uwepo wa majeshi ya Russia huko Venezuela limezungumziwa katika mkutano huu na Washington imekariri msimamo wake wakati wa kujadiliwa suala hilo juu ya udharura wa kuondoka vikosi hivyo vya Moscow huko Venezuela.

Kwa mtazamo wa Beijing na Moscow ni kuwa, hatua za sasa za Marekani dhidi ya Venezuela ni kuanza mwenendo wa kukabiliana na nchi nyingine za Amerika ya Latini zenye tawala za mrengo wa kushoto kama Cuba na Nicaragua ni kwa sababu hiyo basi, jamii ya kimataifa inapaswa kusimama na kukabiliana kwa nguvu zake zote za mienendo hii ya kimabavu ya serikali ya Marekani.

Tags