Zarif azuru Uturuki kujadili masuala ya Syria na Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52902-zarif_azuru_uturuki_kujadili_masuala_ya_syria_na_libya
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitembelea Uturuki kwa ajili ya kujadiliana na viongozi wa nchi hiyo masuala ya uhusiano wa nchi mbili, kurejeshwa amani Syria na vilevile matukio ya hivi karibuni katika eneo la kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2019 03:10 UTC
  • Zarif azuru Uturuki kujadili masuala ya Syria na Libya

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitembelea Uturuki kwa ajili ya kujadiliana na viongozi wa nchi hiyo masuala ya uhusiano wa nchi mbili, kurejeshwa amani Syria na vilevile matukio ya hivi karibuni katika eneo la kaskazini mwa Afrika.

Akizungumza mara tu baada ya kuwasili Ankara mji mkuu wa Uturuki, Zarif amesema kwamba watajadili masuala ya Syria na yale yanayohusiana na eneo la kaskazini mwa Afrika na hasa Libya ambapo kamanda Khalifa Haftar amejaribu kutekeleza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali inayotambulika kimataifa na vilevile Umoja wa Mataifa. Amesema kuwa watajadili masuala yanayozihusu pande mbili yakiwemo ya kiuchumi,ambapo nchi hizi zimekuwa na uhusiano mzuri. Safari ya Zarif nchini Uturuki inafuatia ile aliyofanya Jumanne huko Damascus Syria ambapo alionana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo na kujadiliana nao njia za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita, katika fremu ya mazungumzo ya Astana, mji mkuu wa Kazakhestan.

Zarif (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Rais Bashar Asad wa Syria

Mazungumzo hayo yalianzishwa kwa ubunifu wa Iran, Russia na Uturuki mwezi Januari 2017 kwa ajili ya kuwapatanisha wawakilishi wa serikali na wa makundi ya upinzani kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu wa kudumu nchini Syria. Mazungumzo hayo yanayojulikana kama Mazungumzo ya Amani ya Astana kufikia sasa yamesaidia pakubwa kupunguza mivutano ya kijeshi na ghasia katika nchi hiyo ya Kiarabu kwa kuanzishwa maeneo manne muhimu yasiyo ya kijeshi. Pia yametayarisha mazingira ya kubuniwa Kamati ya Katiba.